Bei mpya ya mafuta Kenya yaandika historia

Nairobi. Bei za mafuta nchini Kenya imepanda kwa kiwango kikubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo, kufuatia ongezeko la gharama za mafuta duniani pamoja na kupanda kwa gharama za usafirishaji duniani.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa jana usiku Aprili 14, 2026 na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli (EPRA), lita moja ya dizeli itaongezeka kwa Ksh40.30 (Sh830) na kufikia Ksh206.84 (Sh4,245), huku petroli ikipanda kwa Ksh28.69 (Sh590) na kuuzwa kwa KSh206.97 (Sh4,250) kwa lita ambapo zitaanza kutumika kuanzia saa sita usiku wa leo Aprili 15,2026.

Bei ya mafuta ya taa itaendelea kubaki Ksh152.78 (Sh3,140) kutokana na ruzuku ya Sh99.16 kwa lita inayotolewa na serikali.

Licha ya serikali kutoa ruzuku ya Ksh20.30 kwa dizeli na Ksh4.92 kwa petroli, ongezeko hilo limechangiwa na kupanda kwa bei za mafuta katika soko la kimataifa pamoja na gharama kubwa za usafirishaji, hasa baada ya kuzuiwa kwa njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta ya kimataifa ya Mlango wa bahari wa Hormuz.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EPRA, Joseph Oketch, amesema serikali imelazimika kupunguza kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kutoka asilimia 16 hadi 13 kwa petroli, dizeli na mafuta ya taa ili kupunguza makali ya bei kwa watumiaji.

“Hatua hii inalenga kulinda watumiaji dhidi ya ongezeko kubwa la gharama za mafuta zinazoagizwa kutoka nje kutokana na kupanda kwa bei katika soko la kimataifa,” amesema Oketch katika taarifa iliyotolewa jana Jumanne usiku.

Taarifa zinaonyesha kuwa gharama ya kuagiza dizeli (ikiwemo usafirishaji) iliongezeka kwa asilimia 68.72 hadi dola 1,073.2 kwa mita ya ujazo, huku petroli ikipanda kwa asilimia 41.53 hadi dola 823.87 na mafuta ya taa yakiongezeka kwa asilimia 105.15 hadi dola 1,311.93 Machi 2026.

Ongezeko hilo linatarajiwa kuongeza mfumuko wa bei na gharama za maisha, huku wazalishaji, watoa huduma na sekta ya uzalishaji umeme wakihamisha gharama hizo kwa watumiaji.

Takwimu zinaonyesha mfumuko wa bei ulipanda hadi asilimia 4.4 mwezi uliopita kutoka asilimia 4.3 Februari.

Wakati huohuo, Waziri wa Nishati wa Kenya, Opiyo Wandayi, alisema mzigo wa mafuta uliokuwa umeagizwa nje ya makubaliano ya serikali kwa serikali (G-to-G), ambao ulikuwa na gharama kubwa, haukujumuishwa katika upangaji wa bei uliotangazwa.

Alisema mzigo huo, uliokuwa na bei ya Ksh198,000 kwa tani moja ya metri, ungeongeza bei ya petroli kwa takriban Ksh14 kwa lita.

Bei hizo mpya zitaendelea kutumika hadi Mei 14, wakati ambapo Kenya na mataifa mengine duniani yakiendelea kuathiriwa na mgogoro wa Mashariki ya Kati.

Ripoti zinaeleza kuwa Iran imekuwa ikishambulia miundombinu ya kusafisha mafuta katika nchi jirani na pia kuzuia usafirishaji kupitia Mlango wa Hormuz, njia ambayo hupitisha takriban asilimia 20 ya mafuta yote duniani.

Kutokana na hali hiyo, bei ya mafuta ghafi aina ya Brent imevuka dola 100 kwa pipa (Sh129,300), huku gharama za bima na usafirishaji nazo zikiendelea kuongezeka.

Imeandikwa kwa msaada wa Daily Nation