JWTZ yatangaza fursa kwa vijana kuanzia kidato cha nne

Dar es Salaam. Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), limetangaza nafasi kwa vijana kuanzia elimu ya sekondari na kuendelea, kuandikishwa katika jeshi hilo.

Vijana watakaoandikishwa Jeshi watapatiwa mafunzo mbalimbali muhimu ya kijeshi na mafunzo ya kuwaendeleza katika taaluma zao.

Taarifa ya nafasi hizo, imetolewa jana, Jumanne Aprili 14, 2026 na kusainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Luteni Kanali Kevin Byabato.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vijana Watanzania na wenye nia ya kuandikishwa wanatakiwa kuwa raia wa kuzaliwa wa Tanzania, umri wa miaka 25 kwa wenye elimu ya kidato cha nne na sita.

Kwa wale wenye elimu ya juu, wanatakiwa kuwa na umri wa miaka isiyozidi 28 na wawe na afya nzuri, akili timamu na tabia na nidhamu nzuri, kadhalika asipatikane na hatia ya makosa ya jinai mahakamani au kufungwa.

Sifa nyingine, anapaswa kuwa na cheti halisi cha kuzaliwa na vyeti vya shule, awe hajatumikia Jeshi la Polisi, Magereza, Chuo cha Mafunzo, Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo au chombo kingine chochote cha ulinzi na usalama.

Pia, anatakiwa awe amehitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mkataba wa kujitolea miaka miwili au mujibu wa sheria na kutunukiwa cheti.

Kwa wale wenye sifa hizo, wanatakiwa kutuma maombi kwa kuandika kwa mkono na kuyawasilisha yalipo Makao Makuu ya Jeshi Msalato Dodoma kuanzia leo Jumatano, Aprili 15 hadi 28, 2026.

Maombi hayo, yametakiwa kuwa na nakala ya kitambulisho cha Taifa au nambari ya utambulisho, nakala ya cheti cha kuzaliwa, vyeti vya shule na chuo na nakala ya cheti cha JKT kwa waombaji waliomaliza mkataba.

Aidha, vijana waliopo kwenye makambi ya JKT hawahusiki na tangazo hilo, pia nambari ya simu ya mkononi ya mwombaji ni muhimu kuambatanishwa.