Usafi unavyofifisha urithi wa biashara ndogo Mji Mkongwe

Zanzibar. Mji Mkongwe wa Zanzibar kwa muda mrefu umebeba taswira ya kipekee iliyojengwa si tu na majengo yake ya kihistoria, bali pia na harakati hai za biashara ndogo ndogo zilizokuwa sehemu ya maisha ya kila siku.

Ndani ya vichochoro vyake na pembezoni mwa barabara, palikuwa na maisha, harufu ya kahawa ya moto, mishikaki inayovutia, muhogo wa kuchoma, bajia, urojo na vitafunwa vingine vya asili vilivyovutia wenyeji na wageni kwa pamoja.

Hata hivyo, sura hiyo imeanza kufifia. Mabadiliko yanayoelezwa kuwa ya kuboresha usafi na mpangilio wa mji yameacha alama ya maswali mengi, hasa kwa wale waliotegemea biashara hizi ndogo kama chanzo chao kikuu cha kipato. Kwa miongo kadhaa, Mji Mkongwe ulikuwa si tu kivutio cha kihistoria bali pia kitovu cha shughuli ndogo za kiuchumi. Kutoka kijiji cha wavuvi mwanzoni mwa karne ya 19, eneo hili lilikuwa kwa kasi na kuwa kitovu muhimu cha biashara katika Afrika Mashariki na Kati.

Ukuaji huo haukutokana tu na biashara kubwa, bali pia mchango wa maelfu ya wafanyabiashara wadogo waliotoa huduma na bidhaa za kila siku.

Biashara hizi ndogo ndogo zilikuwa na mvuto wa kipekee. Wageni walivutiwa sio tu na mandhari ya kale, bali pia na uzoefu wa moja kwa moja wa utamaduni wa Zanzibar kupitia vyakula vya asili na bidhaa ndogondogo zinazouzwa mitaani. Kwa wengi, huo ulikuwa utambulisho halisi wa Mji Mkongwe.

Leo, hali imebadilika. Wafanyabiashara wengi wa aina hii wamelazimika kuondoka, huku baadhi wakidai kupokonywa vifaa vyao na kuvunjiwa meza zao.

Wengine waliokuwa wakitoka vijijini kuja kuuza bidhaa ndogo kama mafuta ya nazi na bidhaa za nyumbani, nao hawana tena nafasi katika mfumo mpya wa biashara.

Badala yake, kinachoonekana kutawala sasa ni biashara zinazolenga watalii pekee, hasa uuzaji wa vinyago na michoro. Ingawa bidhaa hizi zina nafasi yake katika sekta ya utalii, hazitoshelezi kuwakilisha kwa ukamilifu utamaduni mpana wa Zanzibar, hususan ule wa vyakula na maisha ya kila siku ya wananchi wake.

Malalamiko kuhusu hali hii yamefika hadi ndani ya Baraza la Wawakilishi. Kwa upande wao, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Soraga, pamoja na viongozi wa Mamlaka ya Mji Mkongwe, wameeleza kuwa hatua zinazochukuliwa zina nia njema ya kuweka mazingira safi na yenye mpangilio bora zaidi.

Hata hivyo, hoja ya msingi inayojitokeza ni kama usafi na mpangilio huo vinapaswa kuja kwa gharama ya kuondoa vyanzo vya kipato kwa mamia ya wananchi.

Ni wazi kuwa hatua hizi zimewaacha wengi katika hali ngumu ya kiuchumi, wakikosa mbadala wa haraka wa kujikimu.

Kwa takwimu, Zanzibar inakadiriwa kuwa na zaidi ya wafanyabiashara wadogo 30,000 wanaoajiri takriban watu 100,000.

Hili ni kundi kubwa ambalo mchango wake katika uchumi hauwezi kupuuzwa. Ongezeko la wafanyabiashara hawa, sambamba na upungufu wa maeneo ya kufanyia biashara, limezidisha changamoto ya ajira na kipato.

Serikali imefanya jitihada za kujenga masoko ya kisasa, jambo linalostahili pongezi. Hata hivyo, malalamiko kuhusu ugawaji wa vizimba yanaendelea, huku baadhi ya wafanyabiashara wa awali wakidai kukosa nafasi kutokana na ukosefu wa uwazi na utaratibu unaoeleweka.

Zaidi ya hayo, baadhi ya masoko hayo mapya hayajakidhi matarajio ya watumiaji. Yanadaiwa kukumbwa na changamoto za miundombinu, ikiwemo maji kujaa wakati wa mvua, hali inayodorotesha shughuli za biashara.

Pia, kuna hoja kuhusu uendeshaji wa masoko hayo kukabidhiwa kwa taasisi binafsi kwa utaratibu usioeleweka vyema, jambo linaloongeza sintofahamu miongoni mwa wananchi.

Katika muktadha huu, swali la msingi linaibuka: je, sera za kukuza ajira kupitia kujiajiri zinaendana vipi na hali halisi ya mazingira ya biashara?

Ikiwa wafanyabiashara wadogo wanakabiliwa na vizingiti vya kupata maeneo ya kufanyia biashara, gharama za leseni na ada nyingine, ni kwa namna gani wataweza kustawi? Ni muhimu kwa mamlaka husika kutambua kuwa utalii hauishii kwenye mandhari na bidhaa za kumbukumbu pekee.

Wageni wengi huvutiwa na uzoefu wa maisha ya wenyeji, ikiwamo ladha ya vyakula vya asili na mwingiliano wa kijamii unaopatikana katika biashara ndogo ndogo.

Kwa hiyo, changamoto iliyopo si kuchagua kati ya usafi au biashara ndogo, bali ni kutafuta uwiano unaoruhusu vyote viwili kustawi kwa pamoja. Mji Mkongwe unaweza kubaki safi na wenye mpangilio, huku ukihifadhi uhai wake wa kiuchumi na kitamaduni.

Kwa ujumla, suala hili linahitaji mjadala mpana na hatua za makusudi. Serikali, kwa kushirikiana na wadau, inapaswa kubuni mifumo jumuishi itakayowezesha wafanyabiashara wadogo kuendelea na shughuli zao bila kuathiri hadhi ya mji.

Bila kufanya hivyo, kuna hatari ya kupoteza si tu ajira za maelfu ya wananchi, bali pia urithi wa kipekee unaoufanya Mji Mkongwe wa Zanzibar kuwa tofauti na maeneo mengine duniani.