Bakari Mahundu
April 21, 2026
0 Comments
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mussa Zungu amemuonya Mbunge wa Tunduru Kaskazini Ado Shaibu Ado kwa kuendelea kuzungumza baada ya muda wake kuisha na kuzimwa kipaza sauti na Mwenyekiti wa Bunge.
Pia, Spika Zungu alimkosoa Mbunge huyo kwa kurejea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2023/2024, akisema bado haijajadiliwa na Kamati za Bunge za PAC na LAAC ambazo Ado ni mwenyekiti wake.

Akichangia hotuba ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mh. Ado alidai kuwa zaidi ya Sh trilioni 2.5 zimepotea kutokana na ubadhirifu kwa mujibu wa Ripoti ya CAG 2023/2024. Pia aliibua hoja kuhusu matukio ya utekaji, akitaja kupotea kwa Balozi Humphrey Polepole, mwanachama wa Chadema Deus Soka na wengineo, huku akiitaka Serikali kufanya uchunguzi huru.
Wakati wa mchango wake, Ado alikatishwa mara mbili kwa taarifa kutoka kwa Mbunge wa Kaliua Tama na Waziri Patrobas Katambi. Mwenyekiti wa Bunge Cecilia Pareso alipomtaka kukaa, alijaribu kuomba dakika moja ya ziada kutokana na muda wake kupungua kwa kuingiliwa mara kwa mara.
Spika Zungu alisema anamvumilia Ado kwa kuwa ni Mbunge mpya, lakini akasisitiza kuwa hatua za kinidhamu za kikanuni zinaweza kuchukuliwa endapo tabia hiyo itaendelea.