Global Publishers
April 14, 2026
0 Comments
Askofu wa Kanisa Katoliki nchini Marekani, Robert Barron, amesema Rais wa Marekani Donald Trump anapaswa kumuomba radhi Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Pope Leo XIV, kufuatia kauli kali alizotoa dhidi yake kupitia mitandao ya kijamii.
Akizungumza kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Askofu Barron alieleza kuwa kauli za Trump zilikuwa za kukosa heshima na hazichangii mazungumzo yenye tija.
“Kauli alizotoa Rais Trump kuhusu Papa hazikuwa sahihi na hazina heshima. Hazisaidii kujenga mjadala wenye manufaa,” alisema Barron.
Aidha, alisisitiza kuwa ni haki ya Papa kueleza mafundisho ya Kanisa Katoliki na misingi ya maadili, huku akiongeza kuwa tofauti za maoni zinaweza kuwepo baina ya watu wenye nia njema.

Barron pia alipendekeza kuwepo kwa mazungumzo rasmi kati ya viongozi wa serikali ya Trump na maafisa wa Vatican badala ya kutumia mitandao ya kijamii kushambuliana.
Kauli ya Barron imekuja baada ya Trump kuchapisha ujumbe mkali kwenye mtandao wake wa Truth Social, ambapo alimkosoa Papa Leo XIV akimtaja kuwa “dhaifu katika masuala ya uhalifu” na “hafai katika sera za nje”.
Katika ujumbe huo, Trump pia alidai kuwa kuchaguliwa kwa Papa huyo kulitokana na Kanisa kutaka kuwa na mtu atakayekuwa rahisi kushughulika naye kisiasa, hasa kutokana na uraia wake wa Marekani.
Mbali na hilo, Trump alionesha kutoridhishwa na msimamo wa Papa kuhusu masuala ya kimataifa, ikiwemo Iran na sera za Marekani, huku akisisitiza kuwa anatekeleza yale aliyochaguliwa kuyafanya na wananchi.
Mvutano huo unaongeza sura mpya ya tofauti za kimtazamo kati ya baadhi ya viongozi wa kisiasa na kidini, hasa katika masuala ya maadili, sera za kimataifa na nafasi ya dini katika uongozi wa kisasa.