Bosi ATCL afunguka sababu kusitishwa safari ndege ya mizigo

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), Peter Ulanga, amesema kusimamishwa kwa muda kwa safari za ratiba za ndege yake ya mizigo ni uamuzi uliolenga kuondoa hasara na kuongeza ufanisi wa biashara.

Ulanga amesema hayo wakati Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inayoishia Juni 30, 2025 inaonesha ATCL kuendelea kupata hasara.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Ulanga, anasema mwaka 2025 shirika lilifanya tathmini ya kina ya ratiba zake zote za usafiri, ikiwemo za mizigo, ili kubaini ni maeneo gani yalikuwa yanatoa faida na yapi yalikuwa yanapoteza mapato.

Anasema matokeo ya tathmini hiyo yalionesha wazi kuwa baadhi ya safari za ratiba za ndege ya mizigo zilikuwa hazina tija, hasa kutokana na changamoto ya kukosa mizigo ya kutosha katika safari za kurudi.

“Kwa hiyo mojawapo ya maeneo ambayo tuliona yalikuwa hayatupi faida ni ratiba ambayo ilikuwa inaendelea kipindi hicho. Tukairekebisha, tukaanza kufanya charter flights (utaratibu wa kukodisha), jambo ambalo limetupa faida kubwa katika kipindi cha mwaka 2025,” anasema Ulanga.

Hata hivyo, Ulanga anabainisha kuwa kusimamishwa kwa safari hizo hakumaanishi shirika limeachana kabisa na mpango wa safari za ratiba za mizigo, bali lilikuwa ni hatua ya muda ili kufanya marekebisho muhimu.

Anasema baada ya kufanya tathmini na kuboresha mikakati, ATCL sasa iko tayari kurejea katika safari za ratiba za mizigo kwa umakini zaidi, ikilenga masoko yenye uhakika wa mzigo kama China.

“Mwezi huu wa nne, karibu mwishoni tutaanza safari za ratiba baada ya kufanya tathmini ya ufanisi. Itakuwa inaenda China mara tatu kwa wiki, na maandalizi yanakaribia kukamilika. Tumepata usumbufu kidogo kwa sababu tulitaka kusimama (stopover) Mashariki ya Kati, lakini sasa tutasimama India. Uzuri ni kwamba tumeshafanya mahesabu yetu, tumeona tunaweza kupata faida,” anasema.

Anasema wakati wanasubiri ratiba mpya za kupangwa na biashara ya mzigo wa kukodi katika safari na vituo vya ambavyo wanatoa huduma ya ndege za abiria kwa ratiba, wanaendelea na usafirishaji wa mizigo, akisema kuwa safari za China, Afrika Kusini na Kinshasa zinaleta faida kubwa katika eneo hilo.

“Ndege kama 787 (Dreamliner) inaweza kubeba mizigo hadi tani 35, ambazo ni karibu sawa na ndege ya mizigo ya 777. Lakini hatujaishia kwenye kuongeza ufanisi wa ndege zetu tu. Hivi sasa katika muundo wa taasisi tuna idara ya mizigo ambayo haikuwepo kabla ya mwaka 2025,” anasema Ulanga na kuongeza kuwa idara hiyo inasimamia na kuongeza biashara ya mizigo.

Anasema mwelekeo wa sasa ni kutumia zaidi ndege ya mizigo kwa ajili ya kukodisha kulingana na mahitaji, si kama ndege za kawaida za abiria ambazo ratiba yake inakuwa imepangwa, huku akitolea mfano kuwa mara nyingi ilikuwa ikienda Dubai na kurudi bila mzigo.

“Ndege yetu ya mizigo ilikuwa inakwenda Dubai ambayo ni saa tano, ilikuwa haitengenezi fedha. Tumetoka hapo tumeipeleka Kinshasa mara kwa mara ikawa inatengeneza fedha, lakini sasa kabla haijaondoka tunahakikisha pesa inayoingia kwa kwenda na kurudi inatosha gharama na faida,” anasema.

Hata hivyo,anasema Dreamliner ukipelekwa Mumbai bila mzigo unapoteza pesa, hata kama imejaa abiria unapata hasara, hivyo suala la matumizi sahihi ya ndege litaendelea kuelezewa mpaka watu walielewe, ikiwa ni pamoja na kwa nini kuna mpango wa kufungua safari nyingi za masafa marefu.

CAG, Charles Kichere alisema ATCL kwa mwaka wa fedha 2024/25 ilipata hasara ya Sh191.19 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 108 ikilinganishwa na mwaka uliopita, huku akitaja kupaki kwa ndege ya mizigo kuchangia hasara hiyo.

“Hii inafanya kufikisha jumla ya hasara tangu lianzishwe ya Sh748 bilioni, licha ya kuendelea kupokea ruzuku ya Serikali kwa ajili ya mishahara na gharama za uendeshaji,” alisema.

Kichere alisema hasara hiyo imechangiwa na ongezeko la gharama za uendeshaji zilizofikia Sh675 bilioni, zinazozidi kiwango cha mapato. Hilo ni sawa na ongezeko la Sh134 bilioni.

Alieleza shirika hilo lilifanya safari chini ya matarajio, na njia 87 za safari zilikuwa na wastani wa ujazo wa abiria wa asilimia 57 pekee.

Pia alisema amebaini ndege ya mizigo ya Boeing 767-300F ilitumika kinyume na matumizi yake yaliyokusudiwa, na kufanya asilimia 94 ya safari kuwa za masafa mafupi na kati badala ya safari ndefu zenye mapato makubwa.

Aidha alisema ndege hiyo ilifanya safari nyingi chini ya uwezo wake wa kubeba, na hatimaye ilisimamishwa, huku ikiendelea kugharimu shirika takriban Sh3.54 bilioni kwa ukodishaji na bima bila kuzalisha mapato.

Athari za vitaMashariki ya Kati

Ulanga anasema kinachoendelea Mashariki ya Kati kina athari chanya na hasi, kwani pamoja na kuongeza gharama za mafuta, kimefungua njia mpya za safari za ulimwengu kupitia bara la Afrika, hususan kwa abiria ambao mara nyingi walikuwa wakiunganisha safari zao kupitia Mashariki ya Kati.

“Athari hasi ni ongezeko la bei ya mafuta ambayo yanachangia sehemu kubwa ya gharama za uendeshaji. Mfano kati ya mwaka 2023/2024 na 2024/2025, ongezeko la bei ya mafuta ambalo lilikuwa sio kubwa sana lakini liliathiri mapato yetu kwa Sh52 bilioni,” anasema Ulanga.

Kwa upande wa athari chanya anasema: “Abiria ambao walikuwa wanapita Mashariki ya Kati kwenda Mashariki ya Mbali, India na China sasa wanapita kwenye mashirika yetu.

“Tumeona ongezeko la abiria wa Mumbai, China, ndege zinajaa na sisi tumejibu kwa kuongeza safari. Kuanzia Juni mosi India tutakuwa tunakwenda kila siku na China tumetuma ombi hilo.”

Hata hivyo Ulanga anasema hata kabla ya mgogoro wa Mashariki ya Kati, ATCL ilishaanza kuwa kitovu cha safari za kimataifa, ikipitisha abiria kati ya 200 hadi 300 kwa siku, na kwa ushirikiano na mamlaka ya viwanja vya ndege nchini wanatarajia idadi hiyo kuongezeka.

“Kwa mipango ambayo tunayo tunatarajia kuanzisha terminal (uwanja) mahususi kwa ajili ya ATCL ambayo itasaidia kuliweka shirika kama moja ya vitovu vya kikanda.

“Tunatarajia kuwa na terminal 4, ambayo tukimaliza mradi huo tutahudumia wateja wengi wa kimataifa. Lakini pia tunaangalia namna ya kuzipanga ratiba zetu ili kuongeza mvuto wa Dar es Salaam kama kitovu,” amesema.

Anasema hatua nyingine ni huduma za hoteli kwa abiria wanaosubiri ndege kwa muda mrefu kama wanavyofanya mashirika mengine. Matarajio ni kuwa huduma hizo zitaanza kutolewa hivi karibuni.

Ulanga anasisitiza wataalamu wa ATCL na TAA wapo katika mazungumzo na wanaona utayari wa pamoja, lakini pia utashi wa Rais wa kuona ATCL inakuwa imara, ndiyo maana kuna mpango wa kununua ndege nyingine nane kwa ajili ya shirika ili kuhudumia abiria katika viwanja vipya na kuongeza maeneo ambayo bado huduma zinatolewa.

Ulanga ambaye amekuwepo katika shirika hilo kwa takribani mwaka mmoja na nusu sasa, anasema anavyoiona ATCL leo ni kampuni yenye ndege 16 na vituo 32, lakini anatamani kuiona ikiwa na ndege 140–150 ambazo zinaenda sehemu mbalimbali duniani.

“Kama ambavyo mashirika mengine yanafanya kwa nchi zao, natamani kuona shirika likiwa ni sehemu ya nguvu ya kiuchumi ya nchi. Tanzania ni nchi yenye vivutio vingi vya utalii, tunapaswa kuwaleta Watanzania na kuongeza mapato,” anasema.

Anasema matamanio yake ni ATCL kuwa shirika la kiuanamajumui linalochangia maendeleo makubwa ya dunia. Natamani kabla sijaondoka tuweze kwenda hadi Amerika ya Kusini, Ulaya na Marekani na maeneo mengine.