Dar es Salaam. Balozi wa mazingira na mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa TEEMO Africa Company Ltd, Winfrida Shonde ameteuliwa kama mzungumzaji katika kongamano la Uchumi wa Anga za Juu Barani Ulaya 2026, litakalofanyika Mei 5-6, 2026 mjini Lisbon, Ureno.
Kongamano hilo la Uchumi wa Anga za Juu Barani Ulaya 2026, linawakutanisha viongozi wa dunia, wabunifu, watunga sera, wawekezaji na wataalamu kujadili mustakabali wa teknolojia ya anga, matumizi ya data na uwekezaji.
Shonde ambaye pia ni balozi wa mazingira nchini Tanzania atazungumza katika mjadala wa jopo wenye mada “Matumizi ya Takwimu za Anga za Juu katika kuimarisha hatua za Tabianchi”, ambapo atatoa mchango kuhusu namna data za satelaiti zinavyoweza kusaidia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kilimo, ulinzi wa mazingira, na maendeleo endelevu barani Afrika.
Uteuzi wake ni fahari kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla, kwani atakuwa mzungumzaji pekee kutoka Afrika katika mkutano huo, jambo linaloonyesha kuongezeka kwa nafasi ya Afrika katika ubunifu wa mazingira, teknolojia ya anga, na maendeleo endelevu duniani.
Akizungumza kabla ya safari hiyo, Shonde amesema: “Nina heshima kubwa kuiwakilisha Tanzania na Afrika katika mkutano huu muhimu wa kimataifa. Kama Balozi wa Mazingira, ninabeba heshima ya taifa letu na wajibu wa kupeleka sauti ya Tanzania kuhusu hatua za tabianchi na ubunifu.
“Data za anga zinaweza kusaidia sana katika maandalizi ya majanga, kilimo, ulinzi wa mazingira, na mipango ya uwekezaji. Afrika lazima iwe sehemu ya kuunda mustakabali huu,” amesema.
Shonde amekuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira kwa miradi tarajiwa, pamoja na Ukaguzi wa Mazingira kwa miradi mbalimbali nchini, kama sehemu ya takwa la kisheria linalosimamiwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ambapo wawekezaji hupatiwa vyeti vya usajili baada ya kufuata taratibu hizo.
Aidha, amekuwa akihamasisha uhifadhi wa mazingira, suluhisho za tabianchi, ushauri wa ESG na maendeleo ya jamii nchini Tanzania na nje ya mipaka yake. Ushiriki wake unatarajiwa kuongeza hadhi ya Tanzania kimataifa na kufungua fursa mpya za ushirikiano, uwekezaji, na kubadilishana maarifa.
