Tamisemi yaagiza halmashauri nchini kujenga hosteli

Songwe. Halmashauri zote nchini zimetakiwa kuanza kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa hosteli katika shule za sekondari ili kuondoa adha kwa wanafunzi kutembea umbali mrefu.

Lengo ni kuwalinda watoto, hususan wa kike katika mazingira hatarishi pamoja na kupunguza utoro wa rejareja kwa wanafunzi.

Agizo hilo limetolewa Jumatatu, Aprili 20, 2026 na Naibu Katibu Mkuu-Elimu, Ofisi ya Waziri Mkuu- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Atupele Mwambene wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Elimu kitaifa mwaka 2026, inayofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Chiwanda, Momba mkoani Songwe.

Jumla ya mashirika 66 yanashiriki wiki hiyo, yakiwemo ya wanachama 48 wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET).

Mwambene amesema halmashauri zinapaswa kuweka ajenda ya kudumu kwenye vikao kujadili ujenzi wa hosteli, ili kupunguza umbali wa wanafunzi kutembea kutoka nyumbani kwenda shuleni, hali ambayo itakuwa imesaidia kuwaimarishia ulinzi watoto wa kike kuwa na mazingira rafiki ya kusoma.

Amesema ujenzi wa hostel hizo itasaidia kuimarisha mazingira rafiki kujifunzia kwani katika shule nyingi nchini ambazo zimejengewa hosteli ufaulu kwa wanafunzi uko juu ukilinganisha na ambazo hazina hosteli, hivyo ni muhimu kuwekeza kwenye ujenzi huo.

Baadhi ya wananchi wakiwa kwenye viwanja vya shule ya msingi Chiwanda wakifuatilia Uzinduzi wa juma la elimu kitaifa April 20, 2026.Picha na Denis Sinkonde

“Halamsahuri ni lazima muwekeze nguvu kubwa kuwalinda watoto wa kike kwa kiwango kikubwa kwani wapo katika hatari ya kukumbwa na vishawishi vya kuwakatiza masomo pindi wanapotembea umbali mrefu kufuata masomo,” amesema Mwambene.

“Nitoe rai kwa viongozi wa halmashauri kujenga hosteil kwenye shule zilizo mbali sana na makazi ya watu ili wakae karibu na mazingira ya shule, kwanza kutaimarisha ulinzi kwa mtoto wa kike, kuongeza ufaulu na kupunguza utoro na mdondoko wa elimu.

Aidha, amesema kufikia mwaka 2028 Serikali itaanza kutekeleza elimu ya lazima ya miaka 10 na hakutakuwa na ukomo kwa mwanafunzi kuishia darasa la saba, bali wote watafikia kidato cha nne.

Amesema hatua hiyo imeenda sambamba na utekelezaji wa sera ya elimu msingi, ambapo kwa mwaka huu wanafunzi wa darasa la sita na la saba wataenda moja kwa moja kidato cha kwanza.

“Niupongeze mkoa wa Songwe kwa kuwa na ziada ya vyumba 622 vya madarasa ikiwa ni maandalizi ya kupokea wanafunzi katika utekelezaji wa sera ya Serikali ya elimu ya lazima kuanzia mwaka 2028, hivyo niwaombe wazazi kujiandaa na maandalizi ya mazingira ya kupokea wanafunzi kwa mwaka 2028 pamoja na ujenzi wa hosteli,” amesema Mwambene.

Awali, Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Martha Makala amesema maadhimisho hayo ni jukwaa muhimu linalowaunganisha wadau wa elimu kitaifa, likiwa na lengo la kuhakikisha kila mtoto anapata elimu jumuishina yenye usawa.

Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Songwe upande wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Majuto Njanga amesema serikali ya mkoa wa Songwe itaendelea kushirikiana na wadau wa elimu kuhakikisha malengo ya kuboresha elimu yanatimia na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.

Njanga aliyemwakilisha Katibu Tawala amesema watashirikiana na viongozi wa kata na vijiji kuongeza ujenzi wa miundombinu ya madarasa katika shule za msingi za sekondari ili kukabiliana na upungufu unaozikabili.