Dar es Salaam. Wakati wabunge wakipitisha bajeti ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, hoja kuhusu wizara hiyo kuendelea kukosa mfumo imara wa kuratibu rasilimali na programu za vijana, imetawala ndani na nje ya Bunge.
Mjadala huo ulioibuka jana Jumatatu, Aprili 20, 2026 wakati wakijadili bajeti ya wizara hiyo inayoongozwa na Joel Nanauka kwa mwaka 2026/27 ya Sh35 bilioni ambayo ilipitishwa, ulitaka wizara iimarishwe kimuundo na kupewa mamlaka ya kusimamia fedha zote za vijana.
Wizara hiyo mpya ilianzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenda kusikiliza changamoto zao na kuanzishwa Jukwaa la Vijana. Ilianzishwa baada ya baadhi ya vijana kujihusisha na vurugu wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana na kuibua kero za ajira.
Mjadala huo ulipamba moto baada ya mbunge wa Malindi, Muhsin Haji Ussi, kuibua pengo la utekelezaji na kusisitiza umuhimu wa kuiwezesha wizara kifedha ili ijibu changamoto za ajira kwa vijana.
“Kama kuna kitu cha kujivunia Tanzania ni ardhi yenye rutuba, lakini vijana tunakikimbia kilimo kwa sababu hakina soko na teknolojia, nashauri tuunganishe kilimo, usindikaji na elimu ili kufungua ajira,” amesema akisisitiza kuhamishwa kwa Sh200 bilioni za mikopo ya vijana kutoka wizara hiyo na kugawanywa wizara mbalimbali ili kuratibu shughuli zote za vijana.
Hata hivyo, Waziri wa Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka ameweka wazi mkakati wa Serikali kwa wizara hiyo akisema inalenga kuimarisha uwezeshaji wa vijana kupitia maboresho ya sera, mifumo na ushiriki wa sekta binafsi katika kufungua fursa za kiuchumi.
Amesema hatua zimeanza kuchukuliwa kuboresha upatikanaji wa mikopo na mazingira ya biashara kwa vijana ili kuendana na mahitaji halisi ya kundi hilo.
“Kupitia mwongozo mpya, tumepunguza riba hadi asilimia tano, tumeruhusu mikopo ya mtu mmoja mmoja na kutoa muda wa miezi mitatu hadi nane kabla ya marejesho kuanza. Pia, tumeboresha masharti ya dhamana ambapo dhamana sasa ni kifaa kinachokopeshwa badala ya mali zisizohamishika,” amesema.
Pia, amesema wizara itaendelea kuimarisha utendaji wake kupitia ushauri unaotolewa na wadau.
Katika kuendeleza mjadala huo, wabunge walielekeza hoja zao kwenye udhaifu wa muundo wa kifedha na utekelezaji wa programu za vijana, wakisema hali hiyo inapunguza ufanisi wa wizara.
Mbunge wa viti maalumu, Yumma Mmanga Omary amesema mgawanyo wa sasa haukidhi mahitaji ya kundi lililopo chini ya wizara hiyo.
“Asilimia 83 ya fedha zinaenda kwenye uendeshaji huku asilimia 13 pekee ikienda kwenye miradi ya vijana, hali inayoifanya wizara kuwa na fedha kidogo na kupunguza ujumuishi wa kifedha katika wizara. Lazima tuwe na mfumo unaojumuisha vijana wote na kuhakikisha hata wenye ulemavu wananufaika kikamilifu,” amesema.
Katika hali inayoonesha kiu ya wabunge kutaka wizara hiyo kuwekewa mifumo imara ya uratibu wa majukumu yake, hoja hizo zimeibua mjadala mpana zikiungwa mkono na wabunge wengi akiwamo Tina Chenge, aliyesisitiza urahisishaji wa masharti ya mikopo na Elibariki Kingu wa Jimbo la Ikungi, aliyependekeza kuanzishwa kwa kitengo maalumu cha kukuza ujuzi ndani ya wizara hiyo.
Wakati wabunge wakipaza sauti hizo, wataalamu wa sayansi ya siasa na utawala nao wanaungana nao wakisema suluhisho la changamoto zinazoibuliwa katika wizara hiyo zipo kwenye kuijenga kuwa kitovu cha uratibu wa masuala yote ya vijana nchini.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda amesema ili kuondoa matatizo hayo ya kiutendaji na kiuratibu, wizara hiyo inapaswa kuunganisha mifuko, programu na taasisi zote zinazohusu vijana nchini ili kuongeza ufanisi.
“Inapaswa kuratibu na kusimamia mifuko, programu na taasisi zote zinazohusiana na vijana kuanzia ngazi ya Taifa, halmashauri hadi chini kabisa. Hii itaiwezesha wizara kuwafikia vijana na kuwa na mifumo rahisi ya kuratibu na kushughulikia mahitaji ya kundi hili ipasavyo. Tofauti na hivyo, wizara hii haitakuwa na uwezo wa kusimamia vyema majukumu yake na itabaki kama wizara ya kimkakati wa kisiasa tu,” amesema.
Akichambua zaidi, Dk Paul Loisulie wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), amesema wizara hiyo ni ya mtambuko, hivyo inahitaji kuainisha mipaka yake na kupewa uwezo wa kimfumo, kifedha na kitaasisi kusimamia rasilimali zote za wizara hiyo zilizotawanyika katika wizara nyingine.
“Wizara hii inasimamia eneo nyeti, hivyo inapaswa kutambua na kuainisha maeneo mahususi ambayo inashughulika kwa vijana ili isiingiliane na wizara zingine.
“Fedha zilizopo kwenye wizara zingine zinazohusiana na masuala ya vijana zinapaswa kuhamishiwa kwenye wizara hii sasa, ili iweze kuzisimamia na kuratibu shughuli zake moja kwa moja kama Wizara ya Vijana,” amesema Dk Loisulie.
Msomi huyo amesisitiza changamoto zinazoikabili wizara hii zinatokana na msingi kuwa, imeanzia katikati wakati bajeti ya 2025/26 ikiendelea kutekelezwa, akiweka wazi inahitaji utashi wa kisiasa ili itemize lengo la kuanzishwa kwake.
“Cha muhimu kinachohitajika ni utashi wa kuwa na wizara hii ambao tayari unaonekana, kwa kuwa imeundwa, pili sasa ni utashi wa kuiwezesha ili ifanye kazi zake ipasavyo,” amesema.
Kwa upande wake, Dk Conrad Masabo wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), amebainisha mafanikio ya wizara hayapaswi kupimwa kwa ukubwa wa bajeti wala muundo wake wa ndani bali kwa ubora na uwiano wa mikakati na bajeti yake.
“Tunapaswa kupima mikakati iliyowekwa kwenye wizara hii na namna inavyojibu matatizo ya vijana. Kazi ya wizara hii ni kuratibu na kuhakikisha kila sekta inachangia maendeleo ya vijana kwa ufanisi.
“Ni kazi ya wizara ya vijana kuratibu fedha za vijana kila sehemu zilipokwenda. Lakini kuhusianisha ukubwa wa bajeti na utatuzi wa matatizo si sahihi kwani wizara inaweza kupewa fedha nyingi na isitatue matatizo, chamsingi hapa ni mikakati iliyopo na namna utekelezwaji wake unavyojibu matatizo yaliyopo,” amesema.
