UDSM yaja na suluhisho upungufu wa ujuzi wahitimu

Dar es Salaam. Wakati malalamiko ya waajiri kuhusu wahitimu kukosa ujuzi laini yakiendelea kushika kasi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeanzisha mpango wa mafunzo kwa vitendo unaolenga kuwajengea wanafunzi uwezo unaohitajika moja kwa moja katika soko la ajira.

Hatua hiyo imekuja Aprili 21, 2026 baada ya chuo hicho kuzindua rasmi Programu ya UDSM-Skillika kwa kushirikiana na Exact Manpower Consulting Ltd, ikiwa ni jitihada za kuziba pengo la muda mrefu kati ya elimu ya darasani na mahitaji halisi ya waajiri.

Uzinduzi huo umefanyika siku chache tangu tafiti mbalimbali, ikiwemo iliyochapishwa katika Jarida la Journal of Educational Management and Policy Issues la Chuo Kikuu cha Dodoma, kuonyesha kuwa ukosefu wa ujuzi laini kama mawasiliano, nidhamu na utatuzi wa changamoto unachangia kwa kiasi kikubwa wahitimu wengi kukosa ajira licha ya kuwa na sifa za kitaaluma.

Akizungumza kwa niaba ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia taaluma, Profesa Rose Upor, Dk Flora Magige amesema mpango huo ni sehemu ya mageuzi ya kimkakati ya chuo katika kuboresha ubora wa wahitimu wake.

Ameeleza kuwa tayari chuo kilishaanza kuweka misingi ya mabadiliko hayo tangu Februari 2024 kwa kuchapisha mwongozo wa Kamati ya Ushauri wa Viwanda, unaolenga kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo na sekta ya umma na binafsi.

“Ushirikiano huu si hiari tena, ni hitaji. Unasaidia kujenga wahitimu wenye uwezo wa kushindana, kuongeza ubunifu na kuhakikisha elimu inaleta tija kwa maendeleo ya taifa,” amesema Dk Magige.

Amesema mpango huo umejengwa katika mfumo wa hatua tatu unaowafuata wanafunzi tangu mwaka wa kwanza hadi wa mwisho wa masomo yao ya chuo kikuu, ukilenga kuwajengea umahiri hatua kwa hatua hadi wanapohitimu.

“Huu ni mchakato endelevu, si mafunzo ya mara moja. Tunataka mwanafunzi aanze kujifunza ujuzi wa kazi mapema na kuukuza kadri anavyoendelea na masomo,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo mshirika, Kaaya Ndenkunde, amesema changamoto ya wahitimu kukosa ujuzi wa vitendo imekuwa ikiathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji na ufanisi katika maeneo ya kazi.

Amesema ingawa elimu ya darasani bado ni muhimu, haitoshi pekee kuhakikisha mafanikio ya mhitimu katika ajira au kujiajiri.

“Waajiri wengi wanasema jambo lilelile wahitimu wanajua nadharia, lakini wanahitaji kuboreshwa katika mawasiliano, uwajibikaji, nidhamu na utatuzi wa changamoto,” amesema Ndenkunde.

Ameongeza kuwa kupitia Skillika, wanafunzi watapimwa kwa umahiri halisi unaoonekana katika vitendo, badala ya kuishia kwenye maarifa ya darasani pekee.

“Tunataka kuona jinsi wanavyofikiri, wanavyowasiliana na kutekeleza majukumu katika mazingira halisi ya kazi,” amefafanua.

Wataalamu wa elimu wameipongeza hatua hiyo wakisema ni ishara kuwa vyuo vikuu vinaanza kujibu kwa vitendo mahitaji ya soko la ajira.

Mchambuzi wa elimu ya juu, Dk Steven Tweve, amesema kwa muda mrefu mfumo wa elimu umejikita zaidi kwenye vyeti kuliko uwezo halisi wa mhitimu.

“Hii ni hatua muhimu. Soko la ajira sasa linathamini kile mtu anachoweza kufanya, si karatasi alizonazo,” amesema.

Amesisitiza kuwa iwapo mfumo huo utaigwa na vyuo vingine, unaweza kusaidia kupunguza ukosefu wa ajira na kuongeza tija kwa wahitimu.

Naye mtafiti wa elimu, Dk Hemed Mvula, amesema kupuuzwa kwa ujuzi wa mahali pa kazi kumeigharimu nchi kwa muda mrefu kupitia uzalishaji mdogo na vipaji vinavyopotea.

“Wahitimu wanaposhindwa kuwasiliana au kufanya kazi kwa timu, hasara yake inaigusa jamii nzima. Kuziba pengo hili ni uwekezaji mkubwa kwa uchumi,” amesema Mvula.

Katika uzinduzi huo, Profesa Beatrice Mkenda amewahimiza wanafunzi kufuatilia tafiti na mijadala ya hivi karibuni kuhusu ajira, akisisitiza kuwa mpango huo ni fursa muhimu kwao kujiandaa na ushindani wa soko la ajira.