KOCHA wa Simba, Steve Barker, ametuma salamu kwamba kikosi chake kipo tayari kwa michezo ya Kombe la Muungano lakini hawaendi Zanzibar kutalii bali wanalitaka kombe.
Simba inatua Zanzibar kesho Jumatano tayari kwa mashindano hayo ambapo, Wekundu hao wa Msimbazi watacheza mchezo wa kwanza keshokutwa Alhamisi dhidi ya Mafunzo kwenye Uwanja wa New Amaan Complex kisiwani hapa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Barker amesema anatua Zanzibar na kikosi kizima cha timu hiyo, ambapo Simba ina kiu ya mataji na wanalitaka kombe hilo la Muungano msimu huu.
Barker ambaye ni mara ya kwanza kushiriki mashindano hayo huku pia akiiongoza Simba katika Kombe la Mapinduzi 2026 na kuishia nusu fainali, amesema kikosi chake kinampa uhakika kwamba wanaweza kulishindania taji hilo na kulichukua na kwamba hakutakuwa na kudharau mchezo wowote.
“Ndio, tupo tayari kwa mashindano ya Kombe la Muungano, tuliwapa wachezaji mapumziko ya siku moja baada ya kutoka kucheza dhidi ya Namungo, sasa akili zetu na nguvu ni kutafuta taji hili,” amesema Barker.
“Tuna kikosi ambacho kimeonyesha kinaweza kukata kiu ya mataji ya klabu hii kubwa, tutakwenda na wachezaji wote ambao tunawatumia sasa, tuna nguvu ya kutosha kuhakikisha kila mchezo tunacheza kwa umakini na kufika fainali na kutafuta uwezekano wa kuchukua kombe.
Aidha Barker amesema kutakuwa na mabadiliko yanayotokana na ‘rotesheni’ kwa wachezaji wake akitaka kuwapa nafasi wengine lakini akiwahakikishia mashabiki wa simba kwamba timu itakayocheza itakuwa na ushindani.
“Tuna wachezaji wengi wazuri hapa, bahati nzuri tunatoka kwenye ligi, nilisema kabla kwamba huwezi kuchukua ubingwa na wachezaji 11 tutakuwa na rotesheni lakini sio kwa nafasi kubwa sana.
“Tunataka kuhakikisha kila mchezaji anakuwa tayari kuipigania Simba na kushinda, tutakuwa tunakwenda tukiangalia ubora wa mpinzani aliye mbele yetu, kitu muhimu hapa ni kushinda na kwenda kuchukua ubingwa,” amesema.
Mara ya mwisho Simba kulichukua taji hili ilikuwa mwaka 2024 ilipoichapa Azam FC kwa bao 1-0 likifungwa na aliyekuwa kiungo wa timu hiyo, Babacar Sarr. Simba ilikuwa ikinolewa na kocha Abdelhack Benchikha.
