DC Kilombero aagiza watendaji kusimamia kazi ya ugawaji, matumizi ya vyandarua

Morogoro. Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya amewaagiza watendaji wa kata, vijiji na mitaa kuhakikisha kila mwananchi aliyeandikishwa kupata chandarua kwenye halmashauri ya mji Ifakara anapata chandarua hicho bure ikiwa ni jitihada za Serikali katika kutokomeza ugonjwa wa maralia hapa nchini.

Kyobya ametoa agizo hilo wakati akizindua shughuli ya ugawaji wa vyandarua Kwa wananchi wa Halmashauri ya mji Ifakara ambavyo vinasambazwa mkoani Morogoro na Bohari ya Dawa MSD.

Aidha wananchi wa kata 19 walioandikishwa kupata vyandarua hivyo kuhakikisha wanavitumia kwa malengo maalumu yaliyokusudiwa na Serikali ambayo ni kutokomeza na maambukizi ya malaria ambapo amekemea tabia ya baadhi ya wananchi kuchukua vyandarua hivyo na kwenda kufugia kuku ama kuvulia samaki.

“Jumla ya kaya zilizoandikishwa ni 80,000 zenye zumla ya watu 316,000 tuhakikishe wananchi hawa wanapata vyandarua kwa kadri ya walivyojiandikisha,” amesema Kyobya.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara, Pilly Kitwana amesema vyandarua hivyo vinatolewa bure na kwa kiasi kikubwa vitapunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria hivyo amewataka wananchi kuvitumia kwa ajili ya kujikinga na sio kwa shughuli nyingine tofauti.

“Kipekee nimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi wa Halmashauri ya mji Ifakara na kuwaletea vyandarua hivi, sisi kama Halmashauri tunaahidi kufuatilia Kwa karibu matumizi ya vyandarua hivi ili visije vikatumika tofauti na kusudi la Serikali,” amesema Kitwana.

Naye mmoja wa wananchi waliopokea vyandarua hivyo Joseph Maganga ameishukuru Serikali kwa kuwajali na kulinda afya za wananchi na kutoa wito kwa wananchi wenzake kuhakikisha kila mtu anatumia chandarua nyumbani kwake kwani gharama itakayotumika kwenye matibabu ya maralia ni kubwa na wanaweza kupoteza maisha Kwa kuwa ugonjwa huo ni hatari hasa kwa watoto.

Vilevile Maganga amewasihi wananchi wenzake kujitokeza kuchukua vyandarua hivyo katika kata zao walizojiandikisha Kwa kuwa Serikali imetumia gharama kubwa kusambaza vyandarua hivyo.