Morogoro. Serikali imetuma timu ya wataalamu kuchunguza chanzo cha maporomoko ya tope yaliyolikumba Kijiji cha Dimilo wilayani Morogoro, huku shule ya msingi ya kijiji hicho ikifungwa kwa muda baada ya kuzingirwa na tope zito lililosababisha uharibifu wa nyumba na mazao.
Hatua hiyo imekuja kufuatia tukio la maporomoko ya tope kutoka Mlima Mongwe katika kitongoji cha Waga, Kata ya Kibungo Juu, Tarafa ya Matombo, yaliyoanza Aprili 16, 2026 na kuendelea kwa vipindi tofauti, yakiacha athari kwa wananchi kadhaa.
Akizungumza na wananchi na waathirika wa tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala amesema Serikali imechukua hatua za haraka ikiwemo kufunga Shule ya Msingi Dimilo ili kulinda usalama wa wanafunzi na walimu.
Maporomoko ya tope kutoka Mlimba Mongwe yakiwa yamesambaa kwenye eneo la shule ya msingi Dimilo iliyopo kata ya Kibungo juu tarafa ya Matombo wilaya ya Morogoro. Picha Hamida Shariff
“Tumefunga shule hii kwa muda hadi hali itakapokuwa salama. Wanafunzi watahamishiwa katika shule za jirani ili waendelee na masomo wakati wataalamu wakifanya uchunguzi wa kina,” amesema Kilakala.
Aidha, amewataka wananchi kuchukua tahadhari zaidi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, akisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapoona viashiria vya hatari.
“Hili si jambo la kubeza, ni muhimu kushirikiana na kuchukua tahadhari ili kuepusha madhara zaidi,” ameongeza Kilakala.
Kilakala ameeleza kuwa licha ya kutokuwepo kwa vifo au majeruhi, athari za tukio hilo ni kubwa, zikiwemo nyumba kubomoka na mazao kufunikwa na tope.
Kutokana na hali hiyo, ameagiza kamati ya maafa ya wilaya kufanya tathmini ya haraka kubaini kiwango cha hasara na kuweka mikakati ya kusaidia waathirika, hususan waliopoteza makazi na mashamba yao.
Akielezea tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Dimilo, Leonard Mkude, amesema maporomoko hayo yalianza ghafla mchana kwa kishindo kikubwa, yakitokea korongoni na kushuka kwa kasi kuelekea makazi ya watu.
Maporomoko ya tope kutoka Mlimba Mongwe yakiwa yamesambaa kwenye eneo la shule ya msingi Dimilo iliyopo kata ya Kibungo juu tarafa ya Matombo wilaya ya Morogoro. Picha Hamida Shariff
“Baada ya kusikia muungurumo mkubwa, tuliona tope likishuka kutoka mlimani na kufunika sehemu ya kijiji ikiwemo shule,” amesema Mkude.
Ameongeza kuwa maporomoko hayo bado yanaendelea kujirudia kila baada ya saa mbili hadi tatu, hali inayoongeza hofu kwa wananchi na kuathiri shughuli zao za kila siku.
Mwenyekiti huyo amesema takribani watu 20 wameathirika kwa kupoteza nyumba au kuharibiwa makazi yao, huku wengine 22 wakipoteza mazao yao mashambani.
