Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limeweka wazi mkakati wake maalumu wa kutumia fursa ya mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji, kwa kuzindua huduma na vifurushi vitakavyochochea ushiriki wa mashabiki wa soka kutoka ndani na nje ya nchi.
Afcon 2027 inatarajiwa kuanza Juni 19 hadi Julai 18 mwaka 2027 katika mataifa ya Tanzania, Kenya na Uganda ikiwa ni mara ya kwanza kwa mataifa hayo ya Afrika Mashariki kuwa wenyeji wa mashindano hayo yenye hadhi ya juu.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Mkurugenzi Mkuu wa ATCL Peter Ulaganga amesema shirika hilo linaona AFCON 2027 kama jukwaa muhimu si tu kwa michezo, bali pia kwa kukuza utalii, biashara na kuitangaza Tanzania kimataifa.
“Kwa kuwa sisi ni nchi wenyeji wa AFCON 2027, ATCL kama shirika la taifa tunataka kuwa mstari wa mbele kuchagiza ushiriki wa Watanzania na wageni kutoka Afrika na duniani kwa ujumla,” amesema.
Alifafanua kuwa tayari ameanza mazungumzo na timu yake ya wataalamu kubuni bidhaa maalumu itakayowawezesha mashabiki kufurahia michezo huku wakipata uzoefu wa kiutalii ndani ya Tanzania.
“Tunataka mtu akae Zanzibar, aende kuangalia mpira katika jiji au eneo lolote linalochezwa mechi, kisha arejee Zanzibar kulala. Hii ni sehemu ya bidhaa tunayoiandaa,” amesema.
Kwa mujibu wa maelezo yake, ATCL inajiandaa kuzindua vifurushi maalumu (packages) vitakavyowawezesha wageni kuwa watalii na wakati huohuo kuhudhuria mechi katika miji mbalimbali ambayo michezo ya mashindano hayo itachezwa.
Mbali na hilo, shirika hilo pia lina mpango wa kufanya maboresho ya mwonekano wa ndege zake ndani na nje ili kuendana na mandhari ya AFCON, hatua inayolenga kuitangaza Tanzania kama mwenyeji wa mashindano hayo.
“Tuna mradi wa kuzipa ndege zetu zote mwonekano wa ki-AFCON. Baadhi ya vituo tunavyokwenda ni nchi zenye mapenzi makubwa na mpira kama Ghana na Nigeria. Pia tuna mpango wa hivi karibuni kwenda Abidjan (Ivory Coast), Dakar (Senegal) na Cairo (Misri),” amesema.
Aliongeza kuwa safari hizo zitakuwa sehemu ya mkakati mpana wa matangazo ya kimataifa, ambapo ndege za ATCL zitakuwa kama mabalozi wa kuitangaza Tanzania kama mwenyeji wa AFCON 2027.
“Tunapokwenda katika maeneo kama Zambia, ndege zetu zitakuwa na maandishi yanayoonesha wazi kuwa Tanzania ni mwenyeji wa AFCON. Hii itatoa ishara kuwa tuko tayari kupokea mashindano hayo,” amesema.
Aidha, alibainisha kuwa mkakati huo utaenda sambamba na utoaji wa vifurushi maalumu vya usafiri, utalii na tiketi za mechi, hatua ambayo anaamini italeta uzoefu mpya wa kufurahia soka barani Afrika.
“Tutakuwa na vifurushi maalumu vinavyounganisha safari, utalii na burudani ya mpira. Tunaamini hii italeta namna mpya ya mashabiki kufurahia michezo,” alisisitiza.
Kuhusu uwezo wa shirika hilo, Mkurugenzi huyo amesema ATCL kwa sasa ina jumla ya ndege 16, ambapo 15 ni za abiria na moja ni ya mizigo. Hata hivyo, alieleza kuwa hata ndege za abiria zina uwezo wa kubeba mizigo kupitia mfumo wa ‘belly cargo’.
“Hivyo tuna masoko mawili makuu; soko la abiria kupitia ndege 15 na soko la mizigo linalohudumiwa na ndege zote 16,” alieleza.
Kwa upande wa mtandao wa safari, amesema ATCL kwa sasa inahudumia vituo 32, huku mipango ikiendelea kupanua zaidi mtandao huo. Amesema ndani ya mwezi Aprili watafungua kituo kipya na mwezi Mei wataanzisha safari za kwenda Seychelles, hatua itakayofanya jumla ya vituo kufikia 34.
“Kati ya vituo hivyo, 15 ni vya ndani ya nchi na 17 ni vya kimataifa. Tunaendelea kupanua mtandao ili kuhakikisha tunawafikia abiria wengi zaidi,” amesema.
