Iringa. Manispaa ya Iringa imeandika historia mpya baada ya kusaini mkataba wa ujenzi wa ofisi mpya za halmashauri kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza, hatua inayotafsiriwa kama jitihada za dhati za kuboresha mazingira ya utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mradi huo unaotarajiwa kugharimu kiasi cha Sh4.3 bilioni, utatekelezwa katika eneo la Kihesa Kilolo, ambapo maandalizi ya awali yanaendelea kabla ya kuanza rasmi kwa ujenzi.
Hafla ya utiaji saini imefanyika hivi karibuni ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada, na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Zainab Mlawa, pamoja na madiwani kutoka kata zote za manispaa hiyo.
Akizungumzia ujenzi huo, Ibrahim Ngwada ameeleza kuwa na ofisi mpya ni hatua muhimu katika kuimarisha utawala bora na kuongeza ufanisi wa watumishi wa umma katika kuhudumia wananchi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
“Mradi huu ni kielelezo cha dhamira yetu ya dhati ya kuboresha huduma kwa wananchi wa Iringa, na tunaamini utaleta mapinduzi makubwa katika utendaji kazi wa halmashauri,” amesema Ngwada.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa Zainab Mlawa ameeleza kuwa halmashauri imejipanga kikamilifu kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa viwango vya juu na kukamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika haraka iwezekanavyo.
Zainab amefafanua kuwa ushirikiano na Jeshi la Magereza umechaguliwa kwa kuzingatia uzoefu wao katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa taasisi za umma kwa ufanisi.
“Tunatarajia kuona mradi huu ukikamilika kwa ubora unaokusudiwa na kuwa chachu ya maendeleo ya kiutendaji ndani ya halmashauri yetu,” amesema Zainab.
Wakizungumza na Mwananchi Digital Leo Aprili 21, 2026 baadhi ya Wananchi wa Manispaa ya Iringa wamesema wamepokea taarifa hiyo kwa matumaini makubwa, wakiamini kuwa uwepo wa ofisi mpya utarahisisha upatikanaji wa huduma muhimu na kupunguza baadhi ya changamoto.
Mmoja wa wananchi Aisha Kassian kutoka halmashauri hiyo ameleza matarajio yake akisema,
“Tunaamini ofisi hizi mpya zitaleta mabadiliko makubwa, na eneo lile litakuwa kubwa zaidi tofauti na sasa.”
Aidha, wananchi wengine wamesisitiza umuhimu wa usimamizi makini wa mradi huo ili kuhakikisha fedha zilizotengwa zinatumika ipasavyo na mradi unakamilika bila kuchelewa.