Dk Nchemba kuongoza mkutano wa hatma ya uchaguzi wa ALAT Taifa kesho Arusha

Arusha. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba anatarajiwa kufungua na kushuhudia mkutano mkuu wa uchaguzi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) utakaofanyika kesho Aprili 22, 2026 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC).

Mkutano huo wa siku mbili unalenga kupata viongozi wapya wa kitaifa wa ALAT, wakiwemo mwenyekiti, makamu mwenyekiti pamoja na wajumbe wa kamati ya utendaji, kuchukua nafasi ya uongozi unaomaliza muda wake ulioongozwa na Murshid Ngese akisaidiwa na makamu wake, Sima Constantine Sima.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 21, 2026 jijini Arusha, Kaimu Katibu Mkuu wa ALAT, Thomas Vungwa, amesema maandalizi yote ya mkutano huo yamekamilika na unatarajiwa kuhudhuriwa na wajumbe kutoka halmashauri zote 184 nchini.

Amesema mkutano huo utakaofunguliwa na Waziri mkuu Dr Mwigulu Nchemba, unatarajia kuwapata viongozi wapya waadilifu na wachapa kazi wanatakaosaidia jumuiya hiyo kuleta maendeleo yaliyoasisiwa.

Amesema mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea ulianza Aprili 17, 2026 na unatarajiwa kufungwa rasmi kesho, sambamba na kuanza kwa mkutano huo.

“Uchaguzi huu unahusisha nafasi za mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wa Kamati ya Utendaji.Tunatarajia ushiriki mkubwa wa wajumbe wote kutoka mamlaka za serikali za mitaa,” amesema Vungwa.

Benki ya NMB ikiwa mdhamini mkuu wa mkutano huo, imekabidhi hundi ya Sh100 milioni kusaidia kufanikisha maandalizi na uendeshaji wa mkutano huo.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Baraka Ladislaus, amesema benki hiyo imekuwa mdau muhimu wa ALAT kwa zaidi ya miaka 10, ikichangia zaidi ya Sh 1.5 bilioni katika kudhamini mikutano hiyo.

“Ushirikiano huu unatokana na kutambua umuhimu wa ALAT katika kusukuma maendeleo ya serikali za mitaa”

” Tutaendelea kuunga mkono juhudi hizi ili kuhakikisha ajenda za maendeleo zinatimia,” amesema Ladislaus.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mkutano huo, Juma Hokororo, amesema kila kitu kiko tayari kwa ajili ya mkutano huo na ameishukuru NMB kwa mchango wake katika kufanikisha maandalizi.

Katika kinyang’anyiro hicho, baadhi ya wagombea wameanza kujitokeza hadharani kueleza dhamira zao akiwemo Meya wa Kibaha, Dk Nicholas Mawazo, ambaye amesema anagombea nafasi ya mwenyekiti kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji na kuifanya ALAT kuwa sauti imara ya wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“ALAT ni chombo muhimu katika kusimamia serikali za mitaa. Ninalenga kuhakikisha kinakuwa daraja madhubuti kati ya wananchi na serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” amesema Mawazo.

Naye Sima Constantine Sima, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa sasa wa ALAT, amesema amechukua fomu kuwania nafasi ya mwenyekiti akilenga kuimarisha uadilifu, kuboresha miongozo na kusimamia maslahi ya madiwani pamoja na wajumbe wa jumuiya hiyo.

“Lengo langu ni kuona wajumbe wote wanajivunia kuwa sehemu ya ALAT na kuhakikisha taasisi hii inafanya kazi kwa ufanisi zaidi,” amesema Sima.