Mahakama yarejesha kesi ya fidia kwa Shose Sinare

Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imeirejesha kesi ya madai iliyofunguliwa na, Shose Sinare dhidi ya mwajiri wake wa zamani, Stanbic Bank Tanzania Limited na ICBC Standard Bank PLC (zamani Standard Bank PLC).

Mahakama hiyo imeirejesha kesi hiyo baada ya Shose kushinda rufaa aliyoikata akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliofuta kesi yake ya madai ya fidia ya Dola za Marekani 34 milioni, akidai kuvunjiwa heshima kwa kumtuhumu kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Uamuzi huo umetolewa na jopo la majaji watatu waliosikiliza rufaa hiyo, Barke Sehel (mwenyekiti wa jopo), Leila Mgonya na Dk Eliezer Feleshi, baada ya kukubaliana na rufaa za Shose kupitia wakili wake Zaharani Sinare, huku ikitupilia mbali rufaa kinzani iliyokatwa na ICBC Standard.

Katika rufaa hiyo ya madai namba 205 ya mwaka 2023, Shose alikuwa anapinga uamuzi wa Mahakama Kuu, kutupilia mbali kesi yake kwa maelezo kuwa haikuwa na mamlaka ya kuisikiliza kwa kuwa mlalamikaji hakubainisha aina ya fidia anayoidai.

Mahakama ya Rufani katika hukumu yake iliyosomwa na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Wanja Hamza Aprili 14, 2026, imetengua uamuzi wa Mahakama Kuu, baada ya kukubalina na sababu mbili za rufaa, ambazo imesema zinatosha kimaliza rufaa bila kujadili sababu nyingine mbili.

Katika hukumu hiyo mahakama imekubaliana na hoja zote za wakili Sinare, kuwa hati ya madai imeeleza wazi kuwa Dola za Marekani 30 milioni anazoziomba mrufani ni fidia ya hasara halisi, kiasi ambacho kiko ndani ya mamlaka ya kifedha ya Mahakama Kuu kusikiliza kesi hiyo.

Imekubalina na Wakili Sinare, kuwa Mahakama Kuu katika kubaini mamlaka yake ya kifedha ilikosea kuangalia na kuzingatia aya moja tu ya madai, aya ya 27 badala ya kuangalia hati ya madai kwa ujumla wake, zikiwemo aya ya 25 na ya 26.

Mahakama hiyo imefafanua kuwa Mahakama Kuu haikuangalia aya za 25 na 26 hati ya madai zinazobainisha kuwa Dola 30 milioni kinajumuisha hasara ya kukosa fursa za biashara Dola 24 milioni na hasara ya mapato ya ajira Dola 6 milioni.

“Ni kanuni iliyokubalika kisheria kwamba, katika kutafsiri hati ya madai au maelezo ya madai, mahakama lazima izingatie madai yote muhimu yaliyomo ili kubaini maana na madhumuni yake halisi,” alisema Naibu Msajili Hamza akisoma hukumu hiyo.

Pia mahakama imetupilia mbali rufaa kinzani ya ICBC iliyokuwa inapinga uamuzi wa Mahakama Kuu ikidai kuwa ilikosea kisheria kuamua kuwa suala la mamlaka ya kieneo linahitaji ushahidi.

Wakili wake Deusidedith Duncan pamoja na mambo mengine alidai kuwa ingawa hati ya madai inaeleza kuwa benki hiyo inafanya shughuli zake duniani kote, haina makazi wala haifanyi shughuli au biashara zake hapa nchini, hivyo haikupaswa kushtakiwa nchini Tanzania bila kibali cha mahakama.

Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake imekubalina na wakili Sinare kuwa kwa mujibu wa hati ya madai, suala hilo halistahili kuwa pingamizi la awali bali ni suala linalohitaji ushahidi wa kulithibitisha.

Kuhusu hoja ya Mahakama Kuu kutokuamua hoja zake nyingine za pingamizi, Mahakama hiyo imekubalina na Sinare kuwa mahakama inapobaini kuwa suala fulani linamaliza shauri lote, haina wajibu wa kuamua hoja nyingine.

“Tunatengua uamuzi wa Mahakama Kuu na kurejesha jalada la shauri la madai Na. 34 la 2016 katika Mahakama Kuu liendelee kusikilizwa kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, tunatupilia mbali rufaa kinzani.”

Awali kesi hiyo ilitupiliwa mbali na Jaji Ilvin Mugeta katika uamuzi wake ulioandaliwa Juni 14, 2019, kufuatia mapingamizi yaliyoibuliwa na walalamikiwa.

Katika uamuzi huo Jaji Mugeta alikubali hoja za benki hizo za mapingamizi yao akisema Standard ilikuwa na wajibu wa kisheria kuripoti tuhuma hizo na kuwa Benki hiyo ina kinga kamili nchini Uingereza ya kutokushtakiwa kwa hatua hiyo.

Pia aliiondoa Stanbic katika dhima ya uwajibikaji katika madai hayo akisema haikufanya jambo lolote la kuifanya kushtakiwa.

Shose alikata rufaa Mahakama ya Rufani, rufaa namba 89/2020 akiwasilisha sababu sita za rufaa.

Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa Septemba 16, 2021 na jopo la majaji watatu waliosikiliza rufaa hiyo, D. Gerald Ndika, Zephrine Galeba na Abrahamu Mwampashi, ilizingatia sababu mbili tu za rufaa ikatengua uamuzi wa Mahakama Kuu

Ilisema kuwa Mahakama Kuu haikuwa sahihi kwani iliacha kuamua pingamizi lililokuwa limeibuliwa na Stanbic, mahakama kutokuwa na mamlaka, ikaibua yenyewe na kuamua hoja ya mlalamikaji kutokuwa na sababu ya madai dhidi ya Stanbic na bila kuwapa wadaawa fursa ya kuijadili.

Hivyo, ilitengua uamuzi wa Mahakama Kuu na ikaamuru jalada la kesi hiyo lirejeshwe Mahakama Kuu ili kesi hiyo iamuriwe kwa mujibu wa Sheria.

Mara hii kesi hiyo ilisikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki ambaye pia aliitupilia mbali baada ya kukubaliana na hoja moja ya pingamizi la ICBC Standard kuwa hati ya madai haikuonesha mamlaka ya kifedha ya mahakama kusikiliza shauri, uamuzi ambao ndio umetenguliwa katika rufaa hii.

Shose alifungua kesi hiyo Februari 2016 kufuatia taarifa ilizozitoa ICBC Standard kwa Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Udanganyifu Rushwa na Uhalifu wa Kifedha ya Uingereza.

Katika taarifa hiyo ICBC Standard ilimtuhumu yeye na wenzake kujihusisha na rushwa katika mchakato wa upatikanaji mkopo wa Dola za Marekani 600 milioni kwa Serikali ya Tanzania kati  ya mwaka 2012 na 2013, uliowezeshwa na  Benki za Stanbic na Standared ya Uingereza.

Benki hizo zilikuwa benki dada, zikimilikiwa na Standard Bank Goup Limited iliyosajiliwa nchini South Africa hadi Februari mosi 2015, Industrial Commercial Bank of China  Limited (ICBC) iliponunua asilimia 60 ya hisa za Standard ndipo ikaitwa ICBC Standard Bank PLC.

Wakati huo, Shose alikuwa Mkuu wa kitengo cha Wateja Wakubwa na Uwekezaji, hadi Juni 2013, alipoacha utumishi.

ICBC Standard ilidai kuwa katika kufanikisha rushwa hiyo ilimhusisha mtu wa tatu, yaani kampuni ya ushauri wa uwekezaji, huduma za uwezeshaji na upatikanaji wa fedha.

Ilieleza kuwa katika mpango huo ada ya kuwezesha upatikanaji mkopo huo iliongezwa kwa asilimia moja ya kiasi cha mkopo husika, kutoka asilimia 1.4 hadi 2.4.

Hivyo asilimia hiyo moja iliyoongezwa ambayo ni Dola 6 milioni (sawa na zaidi ya Sh15 bilioni kwa sasa) ililipwa kwa kampuni hiyo ya Egma kwa madai kuwa ilihusika katika kutoa ushauri upatikanaji mkopo huo.

Katika kesi hiyo Shose anadai kuwa ICBC Standard ilipotosha na kuficha ukweli muhimu, jambo lililoharibu taswira na heshima yake.

Pamoja na mambo mengine anaomba alipwe fidia Dola za Marekani 34 milioni kwa kuharibiwa hadhi, heshima na taaluma yake ya kibenki na kukoseshwa fursa za biashara na kipato cha ajira.