Benki ya Exim Tanzania na Toyota Washirikiana Kurahisisha Upatikananji wa Magari kwa Watanzania

Dar es Salaam, Tanzania, Aprili 21, 2026: Benki ya Exim Tanzania imeingia katika ushirikiano wa kimkakati na Toyota wenye lengo la kufanya umiliki wa magari kuwa rahisi zaidi na nafuu kwa Watanzania.

Kupitia ushirikiano huu, suluhisho maalum la ufadhili wa magari limeanzishwa, likiwwawezesha watu binafsi na biashara kununua magari mapya na yaliyotumika kwa gharama ndogo ya awali Pamoja na muda nafuu wa marejesho unaoweza kufikia hadi miaka sita.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji Saini huo, Mkuu wa Huduma za Benki kwa Wateja Binafsi na wa Kati wa Benki ya Exim Tanzania, Andrew Lyimo, alisema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya Benki kuendelea kutoa suluhisho bunifu na zinazomlenga mteja moja kwa moja.

“Katika Benki ya Exim Tanzania, tunalenga kufanya zaidi ya huduma za Kibenki za kawaida kwa kutoa suluhisho zinazogusa mahitaji halisi ya kila siku ya wateja wetu. Ushirikiano huu na Toyota unatupa fursa ya kurahisisha umiliki wa magari kupitia mipango nafuu ya ufadhili inayopunguza mzigo wa kifedha huku ikiunga mkono mahitaji ya usafiri binafsi na ukuaji wa biashara,” alisema Lyimo.

Kupitia mpango huu, Benki ya Exim itatoa ufadhili wa hadi asilimia 80 ya gharama kwa magari mapya na asilimia 70 kwa magari yaliyotumika, kwa viwango vya riba shindani vinavyokokotolewa kwa mfumo wa salio linalopungua. Huduma hii inapatikana kwa Shilingi za Kitanzania na Dola za Marekani, ikiwa na malipo ya awali kuanzia asilimia 20.

Kifurushi hiki cha ufadhili wa magari kimetengenezwa ili kuwahudumia wateja mbalimbali wakiwemo waajiriwa, wajasiriamali, biashara ndogo na za kati (SMEs), pamoja na makampuni yanayohitaji suluhisho la uhakika la usafiri bila kuathiri mtiririko wa fedha.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Toyota, Meneja Mkuu William Kadiva, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano huo katika kupanua upatikanaji wa magari yenye ubora nchini Tanzania.

“Ushirikiano wetu na Benki ya Exim Tanzania ni hatua muhimu katika kuhakikisha magari ya Toyota yanawafikia Watanzania wengi zaidi. Kwa kuunganisha ubora wa magari yetu na suluhisho nafuu za ufadhili, tunawezesha watu wengi zaidi kumiliki magari yanayotegemewa kwa matumizi ya kila siku na shughuli za kibiashara,” alisema Kadiva.

Wateja wanaweza kupata huduma hii kwa kutembelea tawi lolote la Exim Bank au showroom za Toyota (Automark) kote nchini ili kujionea chaguo zilizopo na kuanza safari ya kumiliki gari.

Ushirikiano huu unaakisi dhamira ya pamoja ya Exim Bank na Toyota ya kuchochea shughuli za kiuchumi, kuboresha usafiri, na kuunga mkono ukuaji wa biashara nchini Tanzania.