Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, Jaji Mkuu mstaafu, Othman Chande amesema ripoti watakayowasilisha hailengi kumshutumu mtu, wala kuingia kwenye eneo la jinai na madai.
Ripoti hiyo itawasilishwa Alhamisi ya Aprili 23, mwaka huu kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni miezi mitano tangu tume hiyo ilipoteuliwa Novemba 20, mwaka jana na kupewa miezi mitatu ya kazi na baadaye kuongezewa siku 63 ambayo zitaisha Aprili 24, 2026.
Rais Samia aliunda Tume hiyo kutokana na matukio ya maandamano yaliyozaa vurugu siku ya uchaguzi wa Oktoba 29, mwaka jana na kusababisha vifo na uharibifu wa mali.
Ukiacha tume hiyo, matukio hayo yamesababisha Tanzania kupokea wageni kutoka taasisi za kimataifa wakilenga kuchunguza matukui hayo.
Mwenyekiti wa Tume Oktoba 29, 2025, Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande (wa pili kushoto) akiwa pamoja na Wajumbe wa Tume hiyo kabla ya kuzinduliwa Novemba 20, 2025 na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Miongoni mwa taasisi hizo ni Jumuiya ya Madola ambayo ujumbe wake uliwakilishwa na Rais mstaafu wa Malawi, Dk Lazarus Chakwera, aliyefanya ziara ya siku nane na kuzungumza na makundi mbalimbali.
Kabla ya Dk Chakwera, Tanzania ilimpokea mwakilishi kutoka Umoja wa Mataifa (UN), Parfait Onanga-Anyanga, aliyefanya ziara ya siku tatu naye akizungumza na makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikali na vyama vya siasa.
Vilevile, Mtandao wa Viongozi Wanawake Afrika (AFLN) chini ya aliyekuwa Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, akiwa ameambatana na aliyekuwa Rais wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde nao umefika nchini na kuzungumza na makundi mbalimbali kuhusu suala hilo.
Akizungumzia kinachotarajiwa, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda amesema uzito wa ripoti hiyo haupo tu kwenye yaliyomo, bali namna itakavyokabiliana na hofu iliyojengeka kwa jamii tangu mwanzo wa mchakato huo.
“Kinachosubiriwa hapa ni kuona kama ripoti itathibitisha wasiwasi wa baadhi ya wadau au itaondoa hofu hizo. Namna Tume ilivyobadili mfumo wa usikilizaji ushahidi ndiyo iliyozalisha mashaka kwa watu,” anasema.
Hata hivyo, mapema mwaka huu, Jaji Chande akiwajibu wanaoikosoa tume hiyo, aliwataka wasiikosoe tume na wajumbe wake, badala yake wasubiri ripoti ndiyo watoe maoni yao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Jumanne Aprili 21, 2026, Jaji Chande amesema tume hiyo imejikita katika kutafuta hoja na si kusema nani kakosea nini, akisisitiza si mamlaka yao kwenda kwenye jinai wala madai.
“Hatumlengi mwenye jinai wala madai; sisi tutasema watu wamedhurika, kwa namna gani, kwa nini na wapi, lakini hatumshutumu yule ambaye amedhuru,” amesema.
Akilifafanua hilo, amesema katika vurugu hizo kuna watu zaidi ya 320 wameripoti polisi kuibiwa na kuchomewa mali zao, akisema kesi hizo zinaendelea na hazina uhusiano na tume.
Katika hatua nyingine amesema ripoti hiyo inatarajiwa kuwekwa hadharani kwa masilahi ya umma na kuwawezesha wananchi kujua uhalisi wa kilichotokea.
Amesema wakati wanaanza uchunguzi waliona kuwa kuna masilahi ya umma na hata kifungu cha sheria kilichotumiwa na mamlaka ya uteuzi kuunda tume hiyo, kinaweka wazi kuhusu masilahi ya umma.
“Hii inatutaka tume tupendekeze ripoti hiyo iwe hadharani na tunatarajia itakuwa hadharani kuelezea mambo muhimu ambayo watu watayaona kwenye ripoti,” amesema.
Amesema tume hiyo imefikiwa na jumla ya watu 63,603 kwa namna mbalimbali, wakiwemo waliokwenda kutoa ushahidi wa matukio hayo na wataalamu waliotumika kushauri.
Watu hao, Jaji Chande amesema Tume imewafikia katika Wilaya 21 na mikoa 11 na mashahidi wengi waliofikiwa ni waathirika wa matukio husika.
Amesema kati ya watu Tume iliokutana nao, 553 wametoa ushahidi kwa kiapo cha maandishi, huku 1,323 wakitoa ushahidi wa kiapo cha ana kwa ana mbele ya tume.
Wengine 4,891, amesema wametoa ushahidi wao kwa njia ya madodoso kwa maana hawakuandika majina yao wala kujulikana na wananchi 1,317 wamehudhuria mikutano ya hadhara ilivyofanywa katika mikoa iliyoathirika.
Jaji Chande, amesema wananchi 56,445 wametuma ushahidi wao kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi na wataalamu 3,505 wa fani mbalimbali wameshiriki kutoa ushauri kwa tume.
Amesema kwa sababu hadidu za rejea zimewataka kubaini baadhi ya mambo ya kitaalamu na tume haikuwa na mtaalamu katika maeneo hayo, imeruhusiwa kuchukua mtu kutoka nje ya tume.
Vikosi vya usalama vikipambana kutuliza ghasia za Oktoba 29, 2025 katika moja ya mitaa ya Jiji la Dar es Salaam. Picha na Mtandao
“Tumetumia wataalamu wa patholojia. Hawa walikuwa wanaangalia ripoti zinazotolewa chini ya sheria ya uchunguzi wa vifo. Baada ya uchunguzi wa vifo (postmoterm), hawa wanaangalia na kusema kifo kimesababishwa na nini,” amesema.
Kwa kuwa matukio yalihusisha matumizi ya silaha za moto, amesema pia tume ilichukua wataalamu wa vilipuzi waliotumika kueleza silaha gani zilizotumika na zimetumikaje.
“Pia, tulikuwa na wachumi kuangalia fedha zimekuaje hapa katikati baada ya matukio. Kuna walioathirika kisaikolojia, hivyo tulichukua wataalamu wa kisaikolojia,” amesema.
Katika uchunguzi huo, amesema maofisa wa hospitali waliwaambia wamefanya kazi kwa saa 72 mfululizo, bila kurudi nyumbani, hawakujua hali za familia zao, hivyo baadhi walikuwa na msongo wa mawazo.
Wataalamu wengine waliotumika, amesema ni wale wa kuthibitisha uhalisi wa picha mjongeo na mnato, ili kubaini zilizopotoshwa.
“Mnafahamu kuna vyombo pia vimetuma picha za satelaiti kwa hiyo tumewatumia pia wataalamu wa kupima uchunguzi wa kijiografia kuangalia kama kweli satelaiti imepigwa, imepigwa na nani kwa kamera gani,” amesema.
Kuna mashahidi walitishwa
Katika maelezo yake, Jaji Chande amesema kati ya mashahidi wote waliopokea ushahidi wao, ni chini ya watano waliokumbwa na vitisho na kwamba waliwekewa ulinzi.
“Wanne au watano imebidi tuwape ulinzi kwa taratibu zinazojulikana za kisheria za kulinda mashahidi ambazo zipo hata kwenye mahakama, ili wawe salama kwa mchango wao mkubwa,” amesema.
Hata hivyo, amesema hakuna idadi kubwa ya mashahidi waliotishiwa, isipokuwa kuliibuka upotoshaji kutoka kwa baadhi watu ili kuwatisha wananchi wasiende kutoa ushahidi.
Ripoti itakavyowasilishwa
Jaji Chande, amesema katika uwasilishaji wa ripoti hiyo itakayokuwa kwa lugha mbili za Kiswahili na Kiingereza, yeye ataongea kisha Rais Samia atazungumza.
“Kama kawaida, mwenyekiti ataongea kwanza, halafu Rais ataongea kuelezea kwa upande wake na ripoti itakuwa na mapendekezo na mkuu wa nchi atakuwa huru kusema na kuamua yapi atayakubali,” amesema.
Amesisitiza ripoti yao inajibu hadidu za rejea na hoja kwamba, kimetokea nini, wamebaini nini na watapendekeza nini na mambo ya kufanya ili Oktoba 29 isijirudie.
Baada ya uwasilishaji wa ripoti hiyo Alhamisi, siku inayofuata, Ijumaa mchana tume na wajumbe wake wote itakutana na waandishi wa habari kujibu maswali yote yatakayohitaji ufafanuzi wa kila kipengele.
Ushiriki na ufuatiliaji wa wadau kutoka Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Madola, unaifanya ripoti hiyo kuwa zaidi ya nyaraka ya ndani, bali kipimo cha namna Tanzania inavyosimamia haki, uwazi na utatuzi wa migogoro yake ya kisiasa, amesema Wakili Alloyce Komba.
Amesema ujio wa wadau hawo wa kimataifa umeongeza imani juu ya uchunguzi na jinsi uchambuzi wa tukio hilo unaoendelea.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Anna Henga bado ana hofu kuwa mazingira ya uteuzi wa Tume yanaweza kuathiri matarajio ya baadhi ya wadau.
“Tunaisubiri ripoti kwa mashaka, tukihofia inaweza kuwa na majibu ya kung’ata na kupuliza. Lakini bado ni nyenzo muhimu ya kufungua hatua nyingine za kitaifa,” anasema.
Hata hivyo, si kila mmoja ana mtazamo wa mashaka. Doyo Hassan Doyo, mmoja wa waliokuwa wagombea urais katika uchaguzi huo kupitia NLD, anaona ripoti hiyo kama fursa ya kuondoa sintofahamu iliyojengeka.
“Tunatarajia kuona ukweli ukiwekwa wazi ili kuondoa hisia zilizopo kwenye jamii. Hili ni jambo muhimu kwa mustakabali wa demokrasia yetu,” anasema.