Waziri wa Ujenzi Ajibu Kauli ya William Ruto Kuhusu Barabara

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega

WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema Tanzania ina mtandao mkubwa zaidi wa barabara kulinganisha na nchi yoyote jirani huku akisifu jitihada za Watanzania kwenye kujenga taifa lao kwa nguvu na maarifa yao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Aprili 20, 2026 Waziri Ulega alisema kwa ujumla Tanzania ina mtandao wa barabara wenye urefu wa takribani kilomita 182,000 huku kilomita takribani 16,000 zikiwa za lami.

Ingawa hakutaja mtu au tukio lolote, maelezo ya Waziri Ulega ni kama yalikuwa majibu dhidi ya madai yaliyotolewa jana na Rais William Ruto wa Kenya kwamba taifa lake lina mtandao mkubwa zaidi wa barabara za lami kulinganisha zilizopo kwenye nchi nyingine zote za jirani kwa pamoja.

“ Wenzetu wamesema wana kilomita 20,000 za lami. Na wanasema kiwango hicho ni kikubwa kuliko barabara za lami zote zilizopo katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Hata hivyo, sisi peke yetu tuna kilomita 16,000. Jirani zetu Uganda wana kilomita 6,100.

“Ukijumlisha tu kilomita za lami za Tanzania na Uganda, tayari unakuwa umevuka kiwango cha lami cha Kenya. Kwa hiyo zile takwimu za kudogosha kuhusu sisi na wenzetu wa Afrika Mashariki hazikuwa sahihi,” alisema.

Akitoa taarifa zaidi, Ulega alisema zaidi ya hizo ambazo tayari zimejengwa, kuna mtandao wa kilomita 5,100 ambazo zinajengwa nchi nzima na tayari kuna mikataba ya ujenzi wa kilomita 3,700 za lami ambazo imesainiwa na inasubiri kuanza kwa ujenzi wake.

“ Jambo zuri zaidi kuhusu Tanzania ni kwamba wakati tunapata Uhuru, tulikuwa na kilomita za lami zisizozidi 600. Zaidi ya kilomita 15,000 tumezijenga wenyewe kwa nguvu zetu.

“ Kuna jirani zetu walikuta wakoloni wamewajengea maelfu ya kilomita za barabara. Sisi waasisi wetu walijua hatuna mjomba wala shangazi wa kutujengea na tumefanya tulichofanya kwa nguvu na maarifa yetu wenyewe, alisema Ulega.

Ulega alikuwa amepewa nafasi ya kuzungumza kwenye tukio la kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa miundombinu ya bonde la Mto Msimbazi unaotarajiwa kugharimu zaidi ya dola milioni 500 (zaidi ya shilingi trilioni moja) na kubadili kabisa mwonekano na mandhari ya jiji la Dar es Salaam.