Unguja/Dar. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inatambua mchango wa mwanamke katika kuleta maendeleo na itaendelea kuboresha mazingira yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla
leo Jumatano, Aprili 15, 2026 katika Jukwaa la Rising Woman 2026, lililofanyika Zanzibar kwa niaba ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.
Jukwaa hilo la kwanza kufanyika visiwani humo, limeandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) wazalishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen, MwanaSpoti na majukwaa mbalimbali ya mitandaoni.
Abdulla amesema hakuna maendeleo ya kweli yanayoweza kupatikana bila ushiriki kamili wa wanawake katika nyanja zote za kijamii na kiuchumi.
Ameeleza mwanamke wa sasa si tu mlezi wa familia, bali ni mhimili muhimu wa uchumi, akichangia kwa kiwango kikubwa katika masoko, kilimo, biashara na hata teknolojia zinazoibuka.
“Serikal inatambua na kuthamini mchango katika kuleta maendeleo nchini, wanawake wote ambao wanapewa nafasi mbalimbali ikiwemo katika vyombo vya kufanyia uamuzi serikalini na katika taasisi binafsi wanafanya kazi kwa ufanisi mkubwa na wanafanya kazi vizuri,” amesema Abdulla.
Hata hivyo, kiongozi huo amekiri kuwepo kwa changamoto zinazowakabili wanawake, akisisitiza umuhimu wa kuzitatua ili kuwawezesha kutumia kikamilifu uwezo wao katika kuharakisha maendeleo ya nchi.
Katika kubadili mtazamo wa jamii, amehimiza kutambuliwa kwa wanawake kama wahusika wakuu wa maendeleo badala ya kuwaona kama wasaidizi.
Ameeleza wanawake wana uwezo mkubwa wa kusimamia shughuli mbalimbali na kuleta mafanikio, hali inayodhihirika katika ustawi wa jamii na sekta nyingine.
Akizungumzia umuhimu wa jukwaa hilo, amesema limeendelea kuwa chachu ya kuhamasisha uongozi wa wanawake, kujenga mitandao ya ushirikiano na kukuza mchango wao katika maendeleo ya Taifa.
“Ni wazi mwanamke wa leo si wa kusubiri msaada, bali ni mbunifu, kiongozi na mbeba dhamira ya mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kisiasa,” amesisitiza.
Abdulla amebainisha SMZ imeainisha maeneo ya kimkakati ya kumuinua mwanamke kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2025 hadi 2030.
Maeneo hayo yanajumuisha kuimarisha mifumo ya uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake, kupambana na ukatili wa kijinsia kupitia kuboresha madawati ya jinsia, pamoja na kuanzisha na kuimarisha mitandao ya wanawake kwa ajili ya kubadilishana maarifa na fursa.
Aidha, amesisitiza kuendelea kuimarishwa kwa ushiriki wa wanawake katika nafasi za uamuzi katika sekta za umma na binafsi, akibainisha wanawake waliopo katika nafasi hizo wanafanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Amesema kupitia Mamlaka ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Serikali imetoa mikopo isiyo na riba yenye thamani ya Sh53.9 bilioni kuanzia mwaka 2022 hadi Machi 2026, hatua iliyowanufaisha kwa kiasi kikubwa wanawake.
Hata hivyo, Abdulla amesema miongoni mwa mambo muhimu ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele ni uwezeshaji wa kifedha.
“Kama kuna jambo ambalo tunalikosa sana ni elimu ya fedha, tukiweza hili basi tutafanikiwa kwa kiasi kikubwa. Mtu wa kawaida anahisi ni namna tu ya kupewa fedha lakini kama unakosa elimu ya fedha huo mradi hauwezi kudumu,” amesema Abdulla.
Awali, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Zawadi Amou Nassor amesema taasisi kama Mwananchi zinatakiwa kuungwa mkono kwani zinafanya kazi kubwa kusaidia wanawake.
Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Rosalynn Mndolwa-Mworia
Ametumia fursa hiyo kuzitaka taaisis zingine kuiga mfano wa kampuni hiyo.
“Taasisi kama hizi zinazofanya kazi nzuri kuwainua wanawake zinatakiwa kuungwa mkono na zingine ziige mfano,” amesema.

