Kafulila Aeleza Kwa Kina Dhana ya Ubia (PPP), Aondoa Mkanganyiko kwa Wananchi

Global Publishers
April 18, 2026
0 Comments

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila, ametoa ufafanuzi wa kina kuondoa mkanganyiko uliopo miongoni mwa wananchi na wadau kuhusu dhana nzima ya Ubia (PPP).

Akizungumza alipokutana na wadau kutoka sekta binafsi jijini Dar es Salaam, Kafulila alieleza kuwa lengo la kuanzishwa kwa sera ya PPP mwaka 2009 na sheria ya mwaka 2010 ilikuwa ni kurekebisha makosa ya kihistoria yaliyofanyika kwenye mikataba ya nyuma, ili kuhakikisha Serikali na mwekezaji wote wananufaika kwa usawa.

Kafulila aliweka wazi kuwa Serikali inaamua kuingia ubia na sekta binafsi kwa sababu kuu tatu, kwanza. Kutumia Mtaji wa Sekta Binafsi , badala ya Serikali kutumia kodi za wananchi pekee, inatumia fedha za wawekezaji kujenga miundombinu ya umma.

Pili, Kupata Teknolojia Sabidhi, Wakati mwingine Serikali inaweza kuwa na fedha, lakini ikaingia ubia ili kupata teknolojia mpya na ya kisasa ambayo inamilikiwa na sekta binafsi.

Na mwisho, Ufanisi wa Kimenijimenti, Tafiti zinaonyesha sekta binafsi ina ufanisi mkubwa zaidi katika uendeshaji biashara kuliko mashirika ya umma. Mwekezaji huletwa kuongeza ufanisi huo ili mradi ulete tija.

Kituo cha Ubia kipo kuhakikisha mikataba hio kufuata kanuni, miongozo na uwazi ili kulinda maslahi mapana ya Taifa.