AFCON 2027: Dk Ashatu Kijaji kukutana na waongoza watalii Arusha

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk Ashatu Kijaji, anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi jijini Arusha mnamo Aprili 18, 2026, ambapo atazungumza na mamia ya waongoza watalii (Tour Guides) wanaoshiriki mafunzo maalum ya kuongeza ujuzi na kuboresha huduma katika sekta ya utalii.

Mazungumzo hayo yanakuja wakati ambapo Serikali imeweka mkakati wa makusudi wa kuunganisha sekta ya utalii na michezo, hususan kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazotarajiwa kufanyika mwaka 2027 katika nchi za Afrika Mashariki (Tanzania, Kenya, na Uganda).

Mafunzo hayo yanayofanyika jijini Arusha, yamelenga kuwanoa waongoza watalii katika nyanja za weledi, maadili ya kazi, na mbinu za kisasa za kutoa huduma kwa wageni. Dkt. Kijaji anatarajia kusisitiza umuhimu wa kundi hilo kama kiungo muhimu (frontliners) kati ya vivutio vya nchi na wageni watakaofurika nchini wakati wa michuano ya AFCON.

“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa kila mgeni atakayekuja Tanzania kwa ajili ya soka mwaka 2027, anapata hamu ya kutembelea vivutio vyetu vya asili. Waongoza watalii lazima wawe tayari kunufaika na fursa hizi kwa kutoa huduma zenye viwango vya kimataifa,” imeeleza sehemu ya taarifa ya awali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.

Tanzania inatarajia kupokea maelfu ya watalii na wapenzi wa soka kutoka ndani na nje ya bara la Afrika. Serikali imekuwa ikifanya maboresho makubwa ya miundombinu, ikiwemo ujenzi wa uwanja mpya wa kisasa wa Dk Samia Suluhu Hassan jijini Arusha, ambao unatarajiwa kuwa kitovu cha michezo na utalii kaskazini mwa nchi.

Kupitia ziara hiyo, Dk Kijaji anatarajia kutoa muongozo wa namna wadau wa utalii wanavyoweza kujipanga katika mnyororo wa thamani, kuanzia usafirishaji, malazi, hadi utoaji wa maelezo ya vivutio, ili kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Aidha, inatarajiwa kuwa Waziri atagusia matumizi ya teknolojia na mifumo ya kidijitali katika kutangaza vivutio vya utalii, ikiwa ni mwendelezo wa programu ya The Royal Tour iliyoanzishwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan, ambayo imeleta mageuzi makubwa katika idadi ya watalii wanaoingia nchini.

Mkutano huo wa Aprili 18, 2026, unatazamwa na wadau wa utalii jijini Arusha kama kichecheo cha kuleta umoja na maandalizi ya mapema kwa ajili ya mashindano makubwa zaidi ya soka barani Afrika.