Dar es Salaam. Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali itamshikisha adabu yeyote atakayesababisha kero ya kuwanyima Watanzania tabasamu.
Ameeleza hayo leo Ijumaa Aprili 17, 2026 wakati akipokea taarifa ya ujenzi wa barabara ya Mbauda-Losinyai na Tanganyika Packers-Losinyai mkoani Arusha yenye urefu wa kilomita 70.
Dk Mwigulu amesema, “Bahati mbaya sisi wafugaji hatuna uoga, wezi, majambazi, wadokozi na wazembe tutakula nao sahani moja. Wale wanaondika (mitandaoni) watadhani watakera kwa kuandika nawaambia sisi tuliokulia jamii za watoto 16 tulianza kukerana kugombania shuka ya kujifunika isiyotosha,” amesema.
Amesema kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Waziri Mkuu atakuwa na majukumu matatu la kuwa na madaraka ya juu ya udhibiti na usimamizi wa majukumu ya Serikali ya kila siku na kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni.
Jukumu jingine ni atatekeleza au kusababisha maelekezo yoyote ambayo Rais ameyataka kutekelezwa.
“Kama mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) kwenye hotuba yake anataka kuachia tabasamu Watanzania, mimi jukumu langu ni kuona Watanzania wanapata tabasamu hilo,”
“Hata kama wakilala kitandani wanang’atwa na kunguni wanakosa tabasamu, jukumu langu kuhakikisha tunaua kunguni wote ili Watanzania walale na kupata tabasamu,” ameeleza Dk Mwigulu.
Novemba 13, 2025 akifungua Bunge la 13, Rais Samia angependa Serikali ya awamu ya sita itakapomaliza muda wake iache tabasamu kwa Watanzania na si vitu vilivyofanyika pekee.
“Naomba Mungu mwisho wa utumishi wa awamu ya sita, usipime kwa vitu vitakavyoachwa bali tupime kwa tabasamu nitakaloliacha kwenye nyuso za Watanzania,” alisema Rais Samia.
Katika utekelezaji wa hilo, Dk Mwigulu amewataka Watanzania kusoma Katiba ambayo haijaeleza Waziri Mkuu kuwa atakuwa anavaa suti kila wakati na kushughulikia itifaki sambamba na kupewa heshima.
“Tutapasua hadi kwenye miamba Watanzania wapate tabasamu, ndiyo na yeyote anayesababisha kero ya kuwanyima Watanzania tabasamu tutamtia adabu ili Watanzania wapate tabasamu,” amesisitiza Dk Mwigulu.
Amesisitiza watu wa aina hiyo hawataitoa Serikali kwenye reli, akieleza kuwa lazima Watanzania wanufaike na nia njema, dira na ndoto njema ya Rais Samia ya kuwaachia tabasamu.
