Morogoro. Watu 13 wamejeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Ifakara kwenda Morogoro kuacha njia, kupinduka na kutumbukia mtoni.
Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia Aprili 16, katika eneo la Daraja Na. 7, Kata ya Mikumi, wilayani Kilosa.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Andrew Kantimbo, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi hilo ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam.
Amesema kati ya majeruhi hao, 10 ni wanaume na watatu ni wanawake, ambao walipatiwa matibabu katika Kituo cha Afya Mikumi na kuruhusiwa baada ya kubainika kuwa hali zao si mbaya.
Kufuatia ajali hiyo, dereva wa basi hilo anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Kamanda Kantimbo amewataka madereva wengine kuzingatia sheria na tahadhari za usalama barabarani, hasa katika kipindi hiki cha mvua kinachosababisha utelezi wa barabara.
