Watanzania waaswa kuepuka siasa za chuki, waelekezwa kuhimiza maendeleo

Geita. Watanzania wametakiwa kuepuka matumizi mabaya ya siasa yanayochochea chuki, vurugu na machafuko, badala yake wazitumie kama chombo cha kusukuma mbele gurudumu la maendeleo kwa manufaa ya taifa.

Wito huo umetolewa leo Ijumaa, Aprili 17, 2026 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Shilabela, mjini Geita.

Kihongosi amesema siasa si uadui, bali ni jukwaa la kujenga hoja na kutangaza sera kwa lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi wote.

“Watanzania hawana sababu ya kununiana au kutokusemeshana kwa misingi ya tofauti za kisiasa. Siasa zinapaswa kutumika kuhimiza maendeleo, si kugawanya jamii,” amesema.

Ameongeza kuwa ni jambo la kushangaza kuona baadhi ya wananchi wakijengeana chuki kutokana na tofauti za kiitikadi, hali ambayo ni tofauti na uhusiano uliopo miongoni mwa viongozi wa kisiasa wa ngazi mbalimbali.

“Mnadhani mimi na Heche (Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche) hatusalimiani? Au mimi na Zitto (Aliyekuwa kiongozi wa ACT-Wazalendo Zitto Kabwe) hatusalimiani? Hapana. Tunakutana, tunasalimiana vizuri, kwa sababu maisha lazima yaendelee. Tofauti zetu zipo kwenye hoja na sera, si uhusiano binafsi,” amesema.

Amesisitiza kuwa siasa zinahitaji utulivu na hoja zenye mantiki, akibainisha kuwa siasa ni sayansi, si chombo cha hasira au uhasama.

“Siasa hazihitaji hasira, siasa ni sayansi. Wakati sisi viongozi wenu tunasalimiana na kushirikiana, haileti mantiki kwa mtu kumchukia au kumnunia mwenzake kwa sababu tu ya tofauti za vyama kama CCM, CUF au ACT. Hiyo siyo siasa. Na kama unaona huwezi kushiriki siasa kwa misingi hiyo, ni vyema ukajikita katika shughuli nyingine,” amesema.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi akihutbia mkutano wa hadhara katika eneo la Shilabela mjini Geita.

Aidha, amewataka Watanzania kutojihusisha na migawanyiko ya kisiasa, bali wajenge mshikamano kwa misingi ya utaifa na kulinda haki zao.

Katika hatua nyingine, Kihongosi amesema CCM ndiyo chama chenye dhamira ya dhati ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu, pamoja na kudumisha amani na mshikamano nchini. Amewahimiza wananchi kuendelea kukiunga mkono chama hicho.

Ameeleza kuwa chama hicho kina mfumo imara wa kuandaa viongozi tangu ngazi za chini, jambo linalowajengea uwezo na uzoefu wa uongozi, tofauti na vyama vingine.

Kuhusu huduma kwa wananchi, Kihongosi amesema CCM itaendelea kusimamia upatikanaji wa huduma bora za msingi, huku akisisitiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma.

“Hatutakubali kiongozi yeyote kuwa sababu ya wananchi kukosa huduma. Tutachukua hatua bila kujali nafasi au jina la mhusika,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuboresha maisha ya wananchi wa mkoa huo.

Amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26, mkoa huo ulitengewa Sh360 bilioni, huku ukitarajiwa kupokea Sh400 bilioni katika mwaka wa fedha 2026/27.

“Hii inaonyesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwaletea wananchi maendeleo na ustawi,” amesema.

Katika mkutano huo, baadhi ya vijana waliomba ufafanuzi kuhusu namna ya kunufaika na mikopo inayotolewa na Serikali.

Joseph Lipondije amesema licha ya kusikia taarifa za uwepo wa fedha hizo, bado hawana uelewa wa namna ya kuzipata.

Naye Agnes Mashauri ametaja changamoto ya ukosefu wa mitaji kwa vijana, akisisitiza umuhimu wa elimu zaidi ili waweze kutumia fursa ya mikopo hiyo.

Kutokana na hoja hizo, Kihongosi amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, kuandaa mikutano na vikao vya kutoa elimu kwa vijana kuhusu namna ya kupata na kunufaika na mikopo hiyo.