Utalii kupaa, Tanzania ikijipanga kuwa mwenyeji Mkutano IPU

Dar es salaam. Wakati Mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) ukiendelea nchini Uturuki, banda la maonesho la Tanzania limekuwa kivutio kwa washiriki, huku wageni wengi wakitembelea kujifunza kuhusu vivutio vya utalii na fursa zilizopo katika sekta hiyo.

Kutokana na kuvutiwa na maelezo hayo, idadi kubwa ya washiriki wameonyesha nia ya kushiriki Mkutano wa 153 wa IPU utakaofanyika mkoani Arusha Oktoba 2026, kwa kujiandikisha mapema kuthibitisha ushiriki wao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana katika mkutano huo unaohudhiriwa pia na Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo na Mbunge wa Ikungi Magharibi, Elibariki Kingu, zaidi ya wabunge 2,000 kutoka mabunge mbalimbali duniani, wakiongozwa na maspika wao, wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo, jambo linalotarajiwa kuongeza hadhi ya Tanzania kimataifa pamoja na kukuza sekta ya utalii na diplomasia ya bunge.

Katika hatua nyingine, mwanamazingira ambaye ni binti mdogo Georgina Magesa amezungumza kwenye Mkutano Mkuu wa 152 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) unaoendelea jijini Istanbul, Uturuki jana Aprili 16, 2026, akiwa ni mgeni maalumu wa mkutano huo.

Magesa alisisitiza umuhimu wa kulinda kizazi cha sasa, hasa kizazi cha Alfa, kwa kuwekeza katika mazingira rafiki, uhifadhi wa uoto wa asili na ulinzi dhidi ya vitendo hatarishi kwa watoto.

“Dunia inahitaji kizazi salama, na kizazi hiki lazima kilindwe sasa na watangulizi wao,” alisema Magesa.

Magesa amesema hayo huku akiwa sambamba na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa nchini Uturuki, Barham Salih.