Ajira 45,000 zaja Utumishi na Utawala Bora ikiomba Sh1.6 trilioni

Dodoma. Serikali imepanga kuajiri watumishi wapya 45,000 kwa mwaka wa fedha 2026/27 katika ikama za taasisi za umma na kutoa vibali vya ajira mbadala vya watumishi 7,124 wa kada mbalimbali.

Hata hivyo, Kamati ya Bunge imependekeza kuwepo maboresho ya mfumo wa ajira kwa kuruhusu waombaji wenye sifa na vyeti vya ngazi mbalimbali kushiriki katika usaili wa nafasi za kazi zinazotangazwa bila kuwekewa vikwazo visivyo vya lazima kwa misingi ya kiwango cha elimu pekee.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete ametoa takwimu hizo leo Ijumaa, Aprili 17, 2026 wakati akisoma hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/27 ambapo ameomba kudhinishiwa jumla ya Sh1.6 trilioni.

Bajeti hiyo ni ongezeko la zaidi ya Sh200 bilioni ukilinganisha na Sh1.4 trilioni za bajeti ya wizara hiyo iliyopitishwa na Bunge kwa mwaka 2025/26 ambayo pia ilibebwa na vipaumbele, ikiwemo ajira kwa watumishi wengi wakiwa kwenye kada ya elimu.

Waziri Kikwete amesema katika bajeti hiyo, watafanya uhakiki na kuidhinisha madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi wa umma kwa taasisi 425, kuhakiki watumishi na kusafisha taarifa za kiutumishi na mishahara katika taasisi 127 zinazotumia Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi (e-Watumishi).

Amesema Serikali imepanga kuidhinisha maombi ya malimbikizo ya mishahara kwa wafanyakazi waliokoma utumishi kutoka kwa waajiri 200, kushughulikia malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi wa kudumu na kusimamia uchakataji wa orodha ya malipo ya mishahara kwa taasisi za umma 510.

Nyingine ni kuwezesha taasisi 35 ambazo hazitumii mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (e-Watumishi) kuanza kutumia mfumo husika; kuanza utekelezaji wa Programu ya Maboresho ya Mfumo wa Utumishi wa Umma yenye mlengo wa wananchi.

“Programu hii itagharamiwa na fedha za ndani na nje kupitia Benki ya Dunia (IDA-21), kuendesha vikao sita (6) vya Kamati ya Maboresho ya Taasisi za Umma (PIC), kuhuisha mfumo wa e-Watumishi kwa kuongeza huduma mtandao na kuhuisha teknolojia ya mfumo huo kufuatana na maoni ya wadau na mabadiliko ya teknolojia,” amesema Kikwete.

Katika taarifa yake, Waziri amesema watakuwa na programu ya uunganishaji wa mfumo wa e-Watumishi na mifumo mingine ya sekta ya umma na sekta binafsi na kusimamia usalama wa mfumo huo na kuwezesha utekelezaji wa mipango ya motisha na miundo ya maendeleo ya utumishi na mishahara iliyoidhinishwa katika taasisi na mashirika ya umma 70.

Amesema kutakuwa na usimamizi wa uzingatiaji wa maadili katika taasisi za umma kupitia njia mbalimbali pamoja na kampeni za kimaadili katika sekretarieti za mikoa miwili na halmashauri 30, lakini watashughulikia malalamiko 3,500 ya kiutumishi na ukiukwaji wa sheria na kanuni.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2026/27, tutafanya ufuatiliaji na kujenga uwezo wa utekelezaji wa mfumo wa e-Utendaji katika taasisi za umma 571, kukamilisha mapitio ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma, Toleo la Tatu la mwaka 2009 na kutafsiri katika lugha ya Kiswahili,” amesema Kikwete.

Wizara pia imetangaza mpango mwingine ni kuendeleza ujenzi wa nyumba ya kiongozi wa kitaifa mstaafu, na kutoa huduma kwa viongozi wa kitaifa wastaafu 21 (viongozi 10 na wajane 11) kwa mujibu wa sheria.

Kwa mwaka 2026/27, wizara hiyo imesema itatoa mafunzo ya kujiandaa kufanya mitihani ya utumishi wa umma kwa watumishi 10,000 ili kuwajengea uwezo wa utendaji kazi na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Bajeti hiyo imegusa uchambuzi wa rufaa 240 na malalamiko 400 ya watumishi wa umma na wananchi huku wakitarajia kutoa mafunzo kwa viongozi 280 wa Serikali juu ya namna ya kushughulikia rufaa na malalamiko ya watumishi wa umma.

Kuhusu rushwa
Waziri amesema kwa mwaka watafanya utafiti wa kitaifa wa hali ya utawala na rushwa nchini, kuimarisha matumizi ya fedha za umma katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha utekelezaji wake unazingatia thamani halisi ya fedha.

Pia, watafanya uchunguzi wa majalada ya tuhuma za rushwa yanayoendelea pamoja na tuhuma mpya zitakazojitokeza, na kuendesha mashauri ya rushwa mahakamani kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka.

Akisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mbunge wa Itigi (CCM), Yohana Msita, ameitaka Serikali iboreshe mfumo wa ajira kwa kuruhusu waombaji wenye sifa na vyeti vya ngazi mbalimbali kushiriki katika usaili wa nafasi za kazi zinazotangazwa.

Msita amesema hatua hiyo itaondoa malalamiko ya kuwanyima wasomi mbalimbali fursa ya kuomba na kupata ajira kulingana na aina ya elimu waliyonayo kadiri watakavyoona inafaa, kwa kuwa kutumia baadhi ya vyeti vyao wanatimiza vigezo na masharti yaliyobainishwa katika tangazo la ajira husika.

Kamati imeitaka Serikali kupunguza utitiri wa mifumo ya kielektroniki kwani inasababisha changamoto kwa watumiaji; badala yake, kupitia Wakala wa Serikali Mtandao (e-GA), ihakikishe inaunganisha mifumo yenye ufanano wa matumizi na majukumu ili kupunguza changamoto ya kuwa na mifumo mingi inayohitaji nywila tofauti.