Wanahabari, mamlaka za usimamizi wateta vikwazo sekta ya habari nchini

Dar es Salaam. Wadau wa habari nchini wamepaza sauti zao kwa mamlaka za usimamizi wakieleza vikwazo vinavyoikabili sekta hiyo, katika mjadala ulioibua hali halisi ya uandishi wa habari nchini.

Hili linakuja katika wakati ambao tasnia ya habari inakabiliwa na shinikizo kutoka kwa wananchi wanaolalamikia kupungua kwa ubora wa maudhui na kushindwa kwa vyombo vya habari kufika pale ambapo ukweli unahitajika zaidi.

Katika warsha iliyoandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo jijini Dar es Salaam, Ijumaa Aprili 17, 2026, kujadili mchango wa vyombo vya habari katika kuchochea amani, umoja, utulivu na maridhiano ya kitaifa, wanahabari na mamlaka wamejadili changamoto na uhai wa taaluma hiyo katika enzi ya mitandao ya kijamii duniani na namna inavyoibua matatizo ya kimaadili na kuathiri ubora wa maudhui.

Kwa miaka ya karibuni, ukuaji wa mitandao ya kijamii umebadili kwa kasi namna taarifa zinavyotengenezwa, kusambazwa na kupokelewa, huku taarifa zisizo rasmi zikisafiri kwa kasi kubwa kuliko zile zilizothibitishwa.

Ndipo mjadala wa warsha hii unapopata uzito wake, ambapo wanahabari wakizungumza mbele ya viongozi wa wizara, mamlaka za Ithibati, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Jeshi la Polisi, wameeleza vikwazo vinavyowakwamisha kutekeleza majukumu yao.

Vikwazo vinavyobana sekta

Miongoni mwa changamoto zilizobainishwa ni ugumu wa kupata taarifa kwa wakati, vitisho kazini na mifumo isiyowajali kiuchumi.

Akichangia mjadala huo, mwandishi kutoka Habari Mpya, Kelvin Kilongosi, ameibua utata wa mikopo kwa watengeneza maudhui akisema masharti yaliyowekwa hayaendani na uhalisia wa wanahabari wengi wa kidijitali.

“Nina blogu ambayo hata mwaka haijamaliza, naombwa niwasilishe bodi ya wakurugenzi na ripoti ya ukaguzi wa fedha. Hivi vitu vinapatikanaje kwa mtu wa aina yangu?” amehoji.

Wanahabari wengine wameeleza kuwa mazingira ya kisheria, hali ya kiuchumi na vitisho kwa baadhi ya viongozi yanawafanya kushindwa kushindana na kasi ya taarifa zisizo rasmi mitandaoni, hali inayochangia kupungua kwa mvuto wa vyombo rasmi vya habari.

Akifafanua namna waandishi wa habari wanavyopitia mazingira magumu kutokana na mifumo dhaifu ya malipo katika vituo vyao vya kazi, Mhariri wa Gazeti la Raia Mwema, Suleiman Msuya amesema kuwa sekta hiyo  inahitaji mazingira wezeshi  ili kufikia malengo ya ubora wa maudhui yanayozalishwa.

“Kwa sasa wandishi wengi wanaonekana wamepoteza matumaini, mifumo ya sheria imekuwa migumu na wanajiona kama wamesahaulika,” amesema mwandishi mkongwe, Rose Mwalimu akihoji katika mazingira haya unamsaidiaje mwandishi huyu ili afanye kazi inayotakiwa.

Mamlaka zajibu kwa msisitizo wa maadili

Kwa upande wake, Serikali kupitia maofisa wake imejibu hoja hizo kwa kusisitiza maadili, uwajibikaji na uandishi wenye kujali athari kwa jamii.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Maelezo, Zamaradi Kawawa, amewataka wanahabari kurejea kwenye misingi ya taaluma, akisisitiza umuhimu wa kulinda amani na mshikamano wa Taifa.

“Zingatieni maadili ili mfanye uandishi wa kimkakati unaolenga kujenga amani, umoja, utulivu na maridhiano ya kitaifa,” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha usalama wa wanahabari pamoja na kupitia upya masharti ya mikopo ili kuwafikia walengwa wengi zaidi, akiahidi kuwa Serikali itaangalia namna ili waandishi wa vyombo vyote si tu wazalisha maudhui, waweze kuomba mikopo hiyo.

Akizungumzia malalamiko ya vitisho, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amesema jeshi hilo linaendelea kuwajengea uwezo askari wake ili kuboresha ushirikiano na wanahabari.

“Kupitia mafunzo yetu tunawasisitiza askari kufanya kazi kwa kushirikiana na wanahabari wanapotekeleza majukumu yao halali,” amesema, huku akibainisha kuwa baadhi ya migogoro hutokana na ukiukwaji wa maadili.

Misime ameahidi kuwa jeshi hilo litaendelea kushirikiana na wandishi wa habari ikiwemo kutoa taarifa za ukweli na kwa hataka kila matukio yanapotokea ili kurahisisha kazi ya wanahabari.

Kwa upande wa udhibiti wa maudhui, Meneja wa Huduma za Utangazaji wa TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka, amesema sheria zilizopo hazizuii ukosoaji bali zinataka uandishi unaozingatia ukweli na athari zake kwa jamii.

“Kukosoa mnaruhusiwa, lakini lazima mzingatie ukweli, na si kila ukweli unapaswa kuandikwa bila kupima athari zake,” amesema.

Onyo dhidi ya upotoshaji mitandaoni

Katika zama za mitandao ya kijamii ambao upotoshaji umeshamiri mitandaoni, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imeonya juu ya hatari ya maudhui yasiyo na maadili.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Patrick Kipangula, amesema ushindani wa umaarufu mtandaoni usiwafanye wanahabari kupoteza misingi ya taaluma.

“Ni muhimu kupima athari za taarifa kwa jamii. Upotoshaji, lugha za chuki na uvunjifu wa faragha ni hatari kwa mshikamano wa Taifa,” amesema.

Katika warsha hiyo, Wadau wamekubaliana kuwa suluhisho la changamoto hizi haliwezi kuwa la upande mmoja.

Wakati wnahabari wanahitaji mazingira rafiki, upatikanaji wa taarifa na maslahi bora, mamlaka nazo zinahitaji kuona uandishi unaolinda amani na mshikamano wa Taifa.

“Uandishi wa habari unaweza kujenga na unaweza kubomoa pia, ni vyema kuzingatia ukweli lakini si kila ukweli unapaswa kuandikwa. Mwandishi lazima upime ukweli huo ukiuandika unaathari gani kwenye jamii kwa wakati huo,” amesema Mhadhiri wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SJMC), Dk Egbert Mkoko.

Amesisitiza kuwa habari zinazohusu migogoro ya kisiasa, kikabila na kidini zinapaswa kuandikwa kwa uangalifu mkubwa ili kuepuka kuchochea matatizo kwa jamii.