Dar es Salaam. Mchango wa sekta binafsi katika uwekezaji wa miundombinu ya mawasiliano umeendelea kuwa nguzo kuu ya mageuzi ya kidijitali nchini huku Serikali ikikiri kuwa hatua hiyo imeongeza upatikanaji wa huduma na kufungua fursa mpya za kiuchumi.
Kupitia uwekezaji katika ujenzi wa minara ya mawasiliano, uendeshaji wa mitambo na ubunifu wa huduma za kidijitali, kampuni binafsi zimechangia kubadili kwa kiasi kikubwa namna wananchi wanavyowasiliana, kufanya biashara na kupata huduma muhimu.
Akizungumza Aprili 17, 2026 kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, Mkurugenzi wa Biashara wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL), Vedastus Mwita, amesema sekta binafsi imekuwa mstari wa mbele katika kusukuma mbele ajenda ya uchumi wa kidijitali.
Mwita ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya kampuni ya Netis Tanzania inayojihusisha na ujenzi wa minara ya mawasiliano.
Amesema uwekezaji huo wa sekta binafsi umeiwezesha Tanzania kusonga mbele katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 pamoja na Mpango wa Uchumi wa Kidijitali, unaolenga kujenga uchumi shindani unaotegemea teknolojia.
“Leo hii huduma za mawasiliano, intaneti na kifedha zimepanuka kwa kasi na kuwafikia wananchi wengi zaidi, ikiwemo maeneo ya vijijini ambayo hapo awali yalikuwa nyuma,” amesema Mwita.
Ameongeza kuwa sekta hiyo pia imechangia kuongezeka kwa ajira, huku baadhi ya kampuni zikiongeza idadi ya wafanyakazi kutoka takribani 120 hadi zaidi ya 300 kutokana na kukua kwa mahitaji ya huduma za kidijitali.
Akitolea mfano kampuni ya Netis Tanzania, Mwita amesema imekuwa na mchango mkubwa katika kujenga minara ya mawasiliano na kutoa ajira kwa vijana wa Kitanzania, hivyo kusaidia kukuza uchumi wa Taifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya NETIS Tanzania Happy Mushi akizungumza na Mkuu wa wilaya ya Ilala Edward Mpogolo wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya kampuni hiyo inayojihusisha na ujenzi wa minara ya mawasiliano.
“Ni uwekezaji wenye tija ambao unahitaji kuungwa mkono ili kuendelea kuleta manufaa kwa wananchi,” amesema Mwita.
Kutokana na mafanikio hayo, Serikali imeahidi kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha mageuzi ya kidijitali yanaendelea kukua na kunufaisha wananchi wengi zaidi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Netis Tanzania, Happy Mushi amesema katika kipindi cha miaka 10 kampuni hiyo imefanikiwa kusaidia kampuni za simu kwa kujenga na kuendesha minara ya mawasiliano, hatua iliyoboreshwa kwa kiwango kikubwa huduma kwa watumiaji.
Amesema juhudi hizo zimewezesha kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo mengi zaidi, hasa vijijini, na hivyo kupunguza pengo la kidijitali.
“Katika miaka hii 10 tumekuwa sehemu ya mageuzi ya sekta ya mawasiliano kwa kupanua miundombinu ili kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye,” amesema Happy.
Ameongeza kuwa uwekezaji huo umechangia pia kukuza huduma za intaneti, mawasiliano ya simu na huduma za kifedha kidijitali, ambazo zimekuwa muhimu katika kuendesha shughuli za kiuchumi na kijamii.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema mawasiliano si anasa tena bali ni hitaji la msingi linalobeba uchumi na maisha ya kila siku ya wananchi, akitaka wadau wa sekta hiyo kuendelea kuimarisha huduma ili ziendane na mahitaji yanayoongezeka.
Amesema mawasiliano yamekuwa kiungo muhimu kinachounganisha familia, hususan kwa watu wanaofanya kazi mbali na makazi yao au kusoma nje ya nchi, akieleza kuwa utulivu wa maisha ya wananchi wengi unategemea uwezo wa kuwasiliana kwa urahisi.
Mbali na hilo, Mpogolo amesema utekelezaji wa majukumu ya Serikali, ikiwemo ukusanyaji wa mapato kwa njia ya mifumo ya kidijitali, unategemea moja kwa moja uwepo wa mawasiliano imara.
“Maeneo kama Kariakoo yameendelea kunufaika na uwepo wa mawasiliano, kwani wafanyabiashara wengi kutoka ndani na nje ya nchi hutegemea mtandao kufanya miamala na kuendesha shughuli zao.
Hata hivyo, kuna upatikanaji hafifu wa mtandao katika baadhi ya maeneo, hasa ndani ya majengo, kuwa kikwazo kinachohitaji ufumbuzi wa haraka,” amesema Mpogolo.