Wachimbaji wadogo Shinyanga wasitisha uzalishaji kisa tozo za halmashauri

Shinyanga. Wachimbaji wadogo wa madini katika migodi midogo iliyopo Kata ya Mwakitolyo, Halmashauri ya Shinyanga, wamesitisha shughuli za uchimbaji kwa zaidi ya wiki mbili sasa kufuatia kuanzishwa kwa tozo mpya ya Sh200,000 kwa kila gari linalotoka na mawe mgodini.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 17, 2026, wachimbaji hao wamesema chanzo kikuu cha kusimamisha shughuli zao ni kuwepo kwa tozo mpya kwa kila gari linalobeba mawe kutoka mgodini, jambo ambalo limezua malalamiko makubwa miongoni mwao.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wilaya ya Shinyanga, Leonard Waziri.

Mchimbaji mdogo wa madini, David Elias amesema hali ya uchumi kwa wachimbaji imeendelea kuwa mbaya kutokana na uzalishaji kutofanyika na kuiomba serikali kuharakisha mchakato wa kutatua suala hilo ili kurejesha shughuli za uzalishaji.

Mchimbaji mwingine, Janeth Ngangula amesema wachimbaji wako tayari kulipa tozo lakini kiwango kilichowekwa cha Sh200,000 ni kikubwa na kuomba kamati iliyopewa kazi ya kupitia upya tozo hiyo kuharakisha mchakato huo.

Frank Moshi amesema kiwango hicho cha tozo wanashauri kipungue na kufikia Sh20,000 kwa gari moja badala ya Sh200,000 ili kiweze kumudu hali halisi ya uzalishaji na gharama za uendeshaji.

Mchimbaji mdogo wa madini Mwakitolyo, Janeth Ngangula akieleza changamoto ya tozo.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wilaya ya Shinyanga, Leonard Waziri amesema ombi lao kwa serikali ni kushughulikia madai yao kwa haraka, ili kupunguza mzigo wa tozo kwa wachimbaji hasa ikizingatiwa kuwa uzalishaji kwa sasa ni mdogo.

Ameongeza kuwa kusimama kwa shughuli za uchimbaji kumeathiri kwa kiasi kikubwa mapato ya wachimbaji pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi zinazotegemea sekta hiyo katika eneo hilo.

Mchimbaji mdogo wa madini Mwakitolyo David Elias akizungumzia tozo

Hadi sasa, zaidi ya wiki mbili zimepita tangu shughuli za uzalishaji kusimama kufuatia kuanza kwa mjadala wa tozo hiyo, huku wachimbaji wakisubiri majibu kutoka kwa kamati iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya, inayojumuisha pande zote ili kutoa uamuzi wa mwisho juu ya suala hilo.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro alikutana na wachimbaji hao na kusikiliza kilio chao kisha kuunda kamati ambayo itapitia upya tozo hiyo ili kufikia muafaka na kumaliza changamoto iliyojitokeza.