Wawili wafariki kwa ajali Moshi, watatu wajeruhiwa

Moshi. Watu wawili wamefariki dunia papo hapo na wengine watatu kujeruhiwa mkoani Kilimanjaro kutokana na ajali iliyohusisha gari dogo aina ya Altezza lililopoteza mwelekeo.

Ajali hiyo imetokea leo jioni, Aprili 17, 2027, katika eneo la karibu na stendi ya mabasi mjini Moshi, wakati waathirika walipokuwa wakiendelea na shughuli zao za kila siku.

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, amethibitisha kutokea ajali hiyo na kusema majeruhi wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi.

“Leo majira ya saa 10:30 jioni kumetokea ajali katika eneo la stendi ya mabasi Moshi mjini, ambapo dereva wa gari aina ya Altezza alishindwa kulimudu gari kutokana na mwendo wa kasi kisha kuwagonga watu waliokuwa eneo hilo,” amesema Mnzava.

Wananchi wakiangalia gari dogo aina ya Altezza lililopoteza mwelekeo na kusababisha vifo vya watu wawili eneo la eneo la karibu na stendi ya mabasi mjini Moshi.

Ameongeza kuwa jumla ya watu watano waliathirika katika ajali hiyo, ambapo wawili wamefariki dunia papo hapo na watatu wamejeruhiwa.

“Majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mawenzi, huku miili ya waliofariki ikihifadhiwa hospitalini hapo,” ameongeza.

Aidha, Mnzava ametoa wito kwa ndugu, jamaa na marafiki wa waliofariki dunia kufika hospitalini kwa ajili ya kutambua miili ya wapendwa wao.

“Tunaomba ndugu wa wahanga wafike hospitali ya Mawenzi kwa ajili ya utambuzi wa miili,” amesema.