Dodoma. Mvutano kati ya Mbunge wa Tunduru (ACT-Wazalendo), Ado Shaibu, na wabunge wa CCM umeendelea kushika kasi wakati wa michango ya hotuba za wizara, hali inayoonyesha juhudi za kupunguza makali ya hoja zake.
Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, mbunge anaruhusiwa kuomba taarifa akiwa amesimama na kupatiwa; hata hivyo, muda wa majadiliano ya mbunge anayechangia hujumuisha pia muda wa wale wanaoomba taarifa.
Leo, Ijumaa, Aprili 17, 2026, Ado alipokuwa akichangia hotuba ya Wizara ya Utumishi na Utawala Bora, alikatizwa mara kadhaa kwa maombi ya taarifa kutoka kwa wabunge wa CCM, akiwemo Mbunge wa Kaliua pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi.
Hii ni mara ya pili kwa mbunge huyo kukumbana na hali hiyo, baada ya tukio kama hilo kujitokeza alipokuwa akichangia hotuba ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, kuhusu maombi ya fedha kwa mwaka 2026/27.
Akichangia bajeti ya Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora iliyowasilishwa na Waziri Ridhiwani Kikwete, Ado alitoa tuhuma kuhusu utekaji wa watu na vitendo vya ufisadi nchini.
Alieleza kutokuwa na imani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), akidai kuwa licha ya kuwepo kwa upotevu mkubwa wa fedha za umma, taasisi hiyo haijaonyesha nguvu ya kutosha katika kupambana na rushwa.
Ado alisisitiza kuwa hoja yake inatokana na wajibu wake wa kupinga rushwa, akirejea ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinazoonyesha kuwepo kwa ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma.
Alitolea mfano uchambuzi wa chama chake wa ripoti ya CAG ya mwaka wa fedha 2023/24, unaoonyesha kuwa Sh2.5 trilioni zilipotea kutokana na ubadhirifu, huku Takukuru ikiokoa Sh14 bilioni pekee.
Mbunge wa Kaliua, Joseph Tama, alimpa taarifa akidai hoja yake haina msingi kwa kuwa Waziri ameeleza juhudi za Takukuru katika kitabu chake. Hata hivyo, Ado alikataa taarifa hiyo.
Aidha, Ado aligusia suala la utekaji, akidai kuwa bado kuna watu wanatekwa na kupotea bila hatua madhubuti za Serikali, na kupendekeza kuundwa kwa Tume Huru ya Kijaji kuchunguza matukio hayo.
Hoja hiyo ilizua mjadala mkali, ambapo wabunge wengi waliomba kutoa taarifa, lakini Mwenyekiti alimpa nafasi Waziri Katambi.
Akijibu, Katambi alisema kuna uchunguzi na kesi mbalimbali za jinai zinaendelea kuhusu matukio ya utekaji, na kudai kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakijiteka wenyewe.
Alimtaka Ado kutumia taaluma yake ya sheria kuelewa kuwa baadhi ya masuala yapo mahakamani au kwenye uchunguzi wa vyombo vya dola, hivyo hayawezi kujadiliwa kwa kina hadharani.
Hata hivyo, Ado hakukubaliana na maelezo hayo, akisisitiza kuwa anachodai ni uchunguzi huru kupitia Tume ya Kijaji, badala ya uchunguzi wa kawaida wa kipolisi.
Kwa ujumla, mwenendo wa hivi karibuni unaonyesha kuwa wabunge wa CCM pamoja na mawaziri wamekuwa wakiingilia mara kwa mara michango ya Ado Shaibu bungeni, hali inayodaiwa kuathiri uwasilishaji wa hoja zake.
