Bugando yafanikiwa kwa mara ya kwanza kupandikiza figo

Mwanza. Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando imefanikiwa kwa mara ya kwanza kupandikiza figo tangu kuanza kwa mchakato huo miaka miwili iliyopita, hatua inayotajwa kurahisisha huduma hiyo kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa.

Bugando inaongeza idadi ya hospitali zinazotoa huduma ya upandikizaji wa figo nchini.

Miongoni mwa hospitali hizo ni Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambayo ndiyo kinara katika utoaji wa huduma za kibingwa nchini na pia ilikuwa ya kwanza kuanzisha upandikizaji wa figo. 

Hospitali nyingine ni Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Dodoma, ambayo ni ya pili nchini kuanza kutoa huduma za upandikizaji wa figo. 

Mkurugenzi Mkuu wa hospitali ya Bugando, Dk Alicia Massenga akizungumzia mchakato wa upandikizaji figo uliofanyika Aprili 16, 2026 hospitalini hapo.

Akizungumza leo Ijumaa Aprili 17, 2026 hospitalini hapo, Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Alicia Massenga amesema mafanikio hayo ni taarifa njema kwa Watanzania wote na wakazi wa Kanda ya Ziwa, akieleza kuwa maandalizi yalichukua muda mrefu lakini hatimaye yamezaa matunda.

Amesema mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano wa karibu kati ya Bugando na Hospitali ya Benjamin Mkapa, huku akiwashukuru pia Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania pamoja na Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa mchango wao katika kufanikisha huduma hiyo.

“Tumeanza kutoa huduma ya upandikizaji wa figo na itakuwa endelevu, sasa tumeanza na hii timu ya Benjamini Mkapa tutaendelea nao kuwahudumia wagonjwa wengine watakaokuja kuhitaji hii huduma,” amesema Dk Massenga.

Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Ndani hospitali ya Bugando, Dk Ladius Rudovick amesema aliyetoa figo na aliyepandikizwa ni mtu na kaka yake, wakiwa na ulinganifu wa zaidi ya asilimia 90, huku hali zao zote zikiendelea vizuri baada ya upasuaji.

Koliman Mauki aliyemchangia kaka yake figo amesema alichukua uamuzi huo baada ya kushuhudia mateso aliyokuwa akipitia ndugu yake.

“Niliona hali aliyokuwa nayo, ndipo nikachukua uamuzi wa kumsaidia ili apate nafasi ya kuendelea na maisha yake ya kawaida,” amesema.

Naye mgonjwa aliyepandikizwa figo, Even Mauki ameishukuru Serikali, hospitali na wataalamu pamoja na ndugu yake kwa msaada huo, akieleza kuwa anaendelea vizuri na ana matumaini ya kurejea katika maisha ya kawaida.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Upasuaji na kiongozi wa timu ya upandikizaji figo kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Masumbuko Mwashambwa amesema maandalizi ya kuanzisha huduma hiyo Bugando yalianza mwaka 2024 ambapo walialikwa kusaidia kuweka mifumo, kutoa mafunzo na kuandaa wagonjwa.

“Kwa kweli tumeshirikiana kwa karibu sana, tumeelimishana, tumefundishana na kuandaa utaratibu mzima wa upandikizaji figo, na hatimaye jana Aprili 16 tumefanikiwa kumpandikiza mgonjwa wetu wa kwanza hapa Bugando,” amesema.

Profesa Mwashambwa amesisitiza kuwa mahitaji ya huduma hiyo nchini ni makubwa, akieleza kuwa takribani wagonjwa 3,400 wako kwenye huduma ya usafishaji damu (dialysis), hali inayomaanisha hata kama upandikizaji ungefanyika kila siku kwa mgonjwa mmoja, ingetumia miaka zaidi ya tisa kumaliza idadi hiyo.

Ameeleza kuwa wagonjwa wa dialysis hukaa kwa takribani saa nne, mara tatu kwa wiki, jambo linalogharimu fedha nyingi, muda na kuathiri maisha yao kwa kiasi kikubwa.

Dk Samson Kichiba, Mkurugenzi wa huduma za upasuaji Bugando amesema wagonjwa wa figo Kanda ya Ziwa ni wengi kutokana na wingi wa watu wanaoishi kanda hiyo akiishukuru Serikali kwa kufanikisha kuwa na wataalamu wakiwemo madaktari bingwa na bingwa bobezi waliosoma kwa juhudi zake na wadau mbalimbali.

“Upandikizaji figo siyo suala dogo kwanza linahitaji gharama kubwa, hivyo basi pamoja na Serikali kuwekeza kwa ukubwa wake kwenye sekta hii ya afya bado tunahitaji wadau pia kujitokeza….kuna watu wengi wenye shida ya figo lakini hawawezi kumudu gharama.

“Pamoja na Serikali tunahitaji pia wadau mbalimbali kuweza kusaidia wagonjwa wenye uhitaji ili pale ambapo mgonjwa anahitaji upandikizaji wa figo isiwe kigezo kwamba amekosa fedha,”amesema