Serikali yatumia Sh65 bilioni kuimarisha uhifadhi wa misitu

Morogoro. Serikali kupitia Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) imetoa ruzuku ya zaidi ya Sh65 bilioni katika miradi ya kuimarisha uhifadhi wa misitu na maendeleo ya jamii ili kukuza uendelevu wa mazingira na uchumi wa kijani.

Hayo yamebainishwa leo Aprili 17, 2026 na Mtendaji Mkuu wa TaFF, Dk Tuli Msuya wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa vikundi vya ufugaji nyuki ambao ni wanufaika wapya wa ruzuku kwa mwaka 2025/2026  pamoja na maofisa misitu wa halmashauri za wilaya hapa nchini.

Dk Msuya amesema fedha hizo zimetolewa kipindi cha miaka 14 tangu kuanzishwa kwa mfuko huo na kuelekezwa  katika miradi 1,382 ambayo inatekelezwa kwenye wilaya zote za Tanzania bara hadi  kufikia mwaka wa fedha 2025/2026.

Amesema Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuweka kipaumbele katika sekta ya misitu kama mhimili muhimu wa uhifadhi wa mazingira kuongeza uzalishaji na kukuza sekta ya utalii kupitia misitu endelevu.

“Mwaka wa fedha 2025/2026, jumla ya miradi 137 imeidhinishwa kupatiwa ruzuku kati ya maombi zaidi ya 400 yaliyowasilishwa na kwamba miradi hiyo inatekelezwa katika wilaya zaidi ya 40 nchini,” amesema Dk Msuya.

Amesema katika shughuli za ufugaji nyuki, mfuko umewezesha uhifadhi wa eneo la misitu lenye ukubwa wa hekta zaidi ya 400,000 na umeshawezesha miradi ya ufugaji nyuki kwa vikundi 912 vilivyopatiwa jumla ya mizinga 40,608 ya nyuki na vifaa vya kuwezesha ufugaji bora wa nyuki.

Ameongeza kuwa shughuli hizo zilizowezeshwa na mfuko zimefanikisha upatikanaji wa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 2,400,000.

“Nisisitize kwa wanufaika wapya wa ruzuku miradi hii si tu inakwenda kuwanufaisha bali inakwenda kuchangia uhifadhi na kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi katika nchi yetu, na hivyo inapswa kutekelezwa kwa umakini mkubwa,” amesema Dk Msuya.

Naye, mkuu wa kitendo cha miradi na mipango katika mfuko huo, Dk John Mbwambo amesema miradi inayoelekezwa ni ya uhifadhi, usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za misitu.

Dk Mbwambo amesema vikundi vya wafugaji nyuki zaidi ya vikundi 79 vimepatiwa mafunzo hayo ili kuwawezesha wanufaika kutekeleza miradi yao ipasavyo wakizingatia vipengele mbalimbali vya mikataba wanaiyoingia kati yao na mfuko.

 Ameeleza kuwa lengo ni kuhaikikisha fedha ya ruzuku inayotolewa ni kodi ya wananchi na inaelekezwa kwenye shughuli mahususi ya kutekeleza hifadhi na uendelezaji wa misitu.

“Huko nyuma tulikuwa tunawapatia ruzuku bila kuwapatia mafunzo na kwamba zilijitokeza  changamoto wakati wa utekelezaji wa miradi wanapoanza walikuwa wanashindwa kuzingatia mambo ya msingi “ amesema Dk Mbwambo .

Dk Mbwambo ametaja maeneo yaliyokuwa na changamoto ni mrejesho wa matumizi ya fedha , uandishi wa taarifa zinazoinesha wanachokitekeleza  na wakati mwingine kutekeleza shughuli ambazo hazikuanishwa katika mikataba walioingia baina yao na Mfuko.

Kwa upande wao, wanufaika wa ruzuku hiyo wamesema mafunzo hayo yamewasaidia kupata uelewa mpana kuhusu usimamizi wa miradi na matumizi sahihi ya fedha za ruzuku walizopata.

Monica Kilihadalu kutoka kikundi cha Mshikamano ‘B’ Gwata’, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, amesema ruzuku waliyoipata itawawezesha kuongeza mizinga ya kisasa ya kufungia nyuki na hivyo kuendelea kujikwamua kiuchumi na kulinda mazingira hasa misitu.

Mwenyekiti wa Mount Livingstone Development Association Tanzania kutoka Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, Octavian Msemakweli amesema pamoja na juhudi za mfuko huo, ameiomba Serikali kuongeza fedha ili vikundi vingi za ufungaji nyuki vinufaike.