DROO ya Robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB inazikutanisha Simba na TRA United ikiwa ni mara ya tatu msimu huu kukutana katika mashindano makubwa mawili, ikiwamo Ligi Kuu Bara, huku Yanga ikikaribishwa na JKT Tanzania katika Uwanja wa Meja Isamuhyo.
Nyota wa zamani wa Simba, Boniphace Pawasa ametaja winga wa TRA United, Ramadhan Salum ‘Chobwedo’ akiwapa angalizo Wekundu wa Msimbazi kujiandaa ipasavyo kukabiliana naye. Chobwedo hucheza winga ya kulia upande ambao atakuwa akikutana na Nickson Kibabage au Anthony Mligo.
Yanga ndiyo bingwa mtetezi wa michuano hiyo mara nne mfululizo, ambapo timu zingine zilizofanikiwa kutinga hatua hiyo ni Singida Black Stars ambayo itakuwa ugenini kukabiliana na Coastal Union, huku Mashujaa ikiikaribisha Azam FC.
Simba na TRA United katika mechi namba 92, msimu huu zimekutana mara mbili katika ligi, ambapo Wekundu wa Msimbazi waliifunga mara moja huku mechi ya mwisho zikitoka suluhu ugenini mjini Arusha, ilhali mechi namba 93 Yanga na JKT Tanzania msimu huu zimekutana mara moja huku mabingwa watetezi wakipata ushindi wa mabao 5-0 katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Kwa upande mwingine hii itakuwa mara ya pili msimu huu kwa Azam FC kukaribishwa na Mashujaa nyumbani ambapo mechi ya mwisho ya ligi iliyozikutanisha timu hizo ilichezwa Machi 19, 2026 na kumalizika kwa suluhu.
Nayo Singida Black Stars inakaribishwa na Coastal Union katika mechi namba 91, lakini zilikutana Machi 2, 2026 katika Ligi Kuu Bara na Coastal kuchezea kichapo cha bao 1-0. Rekodi hizo zinatoa ufafanuzi mzuri kuhusu hatua hiyo ya robo fainali kwani timu zote zina ugumu wake hasa zinapokuwa nyumbani na ugenini.
Baada ya hatua ya robo fainali, nusu itakuwa ya kibabe ambapo itazikutanisha timu nne pekee kabla ya kwenda kwenye kilele cha michuano hiyo. Matokeo ya robo fainali mshindi atakayepatikana kwenye mechi namba 92 atakuwa nyumbani akiikaribisha mshindi kutoka namba 91, lakini 94 pia atamkaribisha 93.
Katika mechi hizo washindi hao wanne wa nusu fainali ndio watakaokwenda kuamua hatma ya ubingwa kwani katika hatua hiyo zitatoka timu mbili pekee.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto alisema mechi hizo zitaanza kuchezwa mwezi ujao, hivyo timu ztote sitakuwa na muda wa kujipanga.
“Timu zitaanza kucheza Mei 17 katika hatua ya robo fainali na viwanja vyote vitakavyochezewa mechi hizo vinajulikana, lakini kwa upande wa nusu bado kwa sababu viwanja vingi vipo kwenye maboresho.
“Fainali itachezwa baada ya mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara ambapo kwa hesabu za haraka itachezwa mwezi Juni, hivyo timu zina muda mrefu wa kujiandaa.”
Mchezaji wa zamani wa Azam FC, Aggrey Morice alisema kuwa “Mechi yoyote ya mtoano huwa si rahisi kabisa, kila mmoja anataka aingie hatua inayofuata.
“Hakuna mpinzani wala kiwanja chepesi kwa sababu timu zote zina viwango bora, kwa hiyo kila mmoja anatakiwa ajipange tu na ugumu utakuwepo.”
Boniphace Pawasa alisema “Timu zote zilizofika hatua hii ni bora na ngumu, ukiangalia Simba inakutana na TRA United ambayo ina mchezaji kama Chobwedo ambaye anasumbua sana kwa sasa.
“Lakini Azam pia tumeiona kwenye mechi iliyopita ilivyopambana sana na Mashujaa kwake kwa hiyo haitakuwa hatua nyepesi kwani timu zote ni ngumu.”
Mwakilishi wa Yanga, Hafidhi Salehe alisema kuwa “Sisi kama mabingwa watetezi tuko tayari na ubingwa tunautaka kwa mara ya tano mfululizo.
“JKT Tanzania ijipange kwa sababu hatutacheza mechi hiyo kawaida ila tutapambana kuhakikisha tunashinda na kutua nusu fainali.”
