JAB yatoa neno kwa wanahabari

Dar es Salaam. Katika zama za utitiri wa taarifa zisizorasmi zinazosambaa kwa kasi kupitia ukuaji wa mitandaoni ya kijamii duniani, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), imetoa mwelekeo unaopaswa kufuata wanahabari nchini ili kuepuka kukumbana na mkono wa sheria.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Patrick Kipangula alipozungumza katika warsha ya wanahabari iliyoandaliwa na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Aprili 17, 2026 jijini Dar es Salaam.

Katika warsha hiyo iliyolenga kuwajengea uwezo wanahabari kuhudu uandishi unalenga kuchochea amani, umoja wa kitaifa, utulivu na maridhiano, Mkurugenzi huyo ametoa nasaha akifafanua wanayopaswa kuepuka wanahabari ili kufikia lengo hilo.

“Waandishi wa habari ni nguzo muhimu kwakuwa ndio hubeba taarifa mbalimbali kutoka Serikalini na vyanzo vingine na kuzipeleka kwa jamii, hivyo ni vyema kuzingatia maadili ya kitaaluma katika kutekeleza majukumu hayo,” amesema.

Kipangula amewaasa waandishi wa habari kuzingatia ukweli na haki katika majukumu yao ili kujilinda wenyewe na kuwalinda wengine.
“Lakini ni muhimu pia kupima athari za ukweli wa taarifa unayotoa kwa jamii,” amesema akikemea vitendo vya kimaadili kama kupokea rushwa na kulinda vyanzo vyao vya habari.
Amesema wajibu wa wandishi wa habari ni kuwajibika kwa wananchi kwa kuwapa habari zinazoaminika, kuwasikiliza na kuzingatia uandishi unaozingatia athari za habari hizo kwa jamii ili kuepuka kuwasababishia madhara watu.

“Mfano imetokea ajali, unaporipoti unapaswa kuripoti stori hiyo katika namna ambayo haileti madhara, pia thibitisha na tunza vyanzo vya taarifa uliyopokea,” amesema.
Amesema habari zinazohusu migogoro ya kisiasa au kikabila na kidini zinapaswa kuripotiwa kwa umakini mkubwa ili kuepusha kuendeleza matatizo zaidi.

Aidha, amesisitiza waandishi kulinda faragha za watu akikumbusha sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi.

“Mfano mtu anamhoji mfiwa anamuuliza unajisikiaje sasa, au mtu anampigia simu mtu aliyefukiwa na kifusi anaulizwa unahitaji msaada, haya ni mambo yanayoongeza hudhuni na usumbufu,” amesema Kipangula.

Pia amekemea uandishi wa maudhui yasiyofaa kwa jamii akigusia masuala ya ushoga na habari za kupotea nyeti.

Aidha, amesema habari za uchumi zinapaswa kuandikwa kwa umakini mkubwa kwa kuzingatia takwimu sahihi ili kuepusha upotoshaji.

“Upotoshaji ni janga sana katika radio za mtandaoni, unaweza kuambiwa fulani amekufa wanaonesha kabisa na jeneza pembeni, halafu yupo salama kabisa, jiulize familia yake wanjisikiaje. Kwanini upate wafuatiliaji kwa kufanganya?,” amesisitiza.

Pia amesema masuala ya kijinsia na kulinda watoto, kuepuka ubaguzi, unyanyapaa na kunyanyasa yanapaswa kuepukwa.
“Matumizi ya lugha au kuripoti taarifa zinazochochea migawanyiko ya kijamii, (hate speech) ni kosa kisheria na inaweza kuleta madhara makubwa kwa jamii, ni muhimu kuepuka ili kulinda umoja wa kitaifa.

“Haki ya kujibu pia ni muhimu kuheshimiwa hasa mtu anapotajwa kwa namna yoyote inayoathiri hadhi yake, ili kuzingatia mizania. Hii ni haki ya asili na usippzingatia unaweza kushitakiwa,” amesema.
Pia amesisitiza kuzingatia matumizi sahihi ya Akili Unde (AI) katika uandishi wa habari ili kuzalisha maudhui yasiyokiuka maadili.
“Tukizingatia haya yote tutakuwa tumerudi kwenye dhana ya kujenga amani, utulivu na maridhiano,” amesema.