Mahakama yaamua nani anastahili kutumia ‘Baby’ kama alama ya biashara

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imemaliza mgogoro wa kugombea alama ya utambulisho wa biashara (trade mark) kati ya Dream Cosmetics na Tanga Pharmaceutical & Plastics Limited.

Mgogoro huo uliibuka baada ya Dream Cosmetics kuwasilisha kwa Naibu Msajili wa Alama za Biashara na Huduma ombi la kusajili jina la “BABYMED”, lakini Tanga Pharmaceutical & Plastics Limited wakapinga wakidai linafanana na jina lao.

Mgogoro huo ulianza Februari 20, 2021, baada ya Dream Cosmetics kuwasilisha kwa Msajili alama ya biashara TZ/T/2021/326 ‘BABYMED’ Class 3, ambayo ilichapwa katika Jarida la Alama za Biashara na Huduma la Juni 15, 2021.

Hata hivyo, Julai mosi, 2021, kampuni ya Tanga Pharmaceutical & Plastics Limited ilipinga kusajiliwa kwa alama hiyo ya biashara kwa maelezo kuwa inafanana na alama yake ya biashara ambayo ilishasajiliwa kama TZ/T/2011/354 ‘BABY & ME’.

Kampuni hiyo ina bidhaa zinazotumia alama ya biashara ya “BABY & ME”, na ilieleza kuwa kama “BABYMED” ingesajiliwa ingewachanganya wateja sokoni, kinyume cha Sheria ya Alama za Biashara na Huduma (Marekebisho ya 2023), kifungu cha 16.

Baada ya kusikiliza hoja za kampuni hizo mbili, Msajili wa Alama za Biashara na Huduma, Seka Kasera, alikubaliana na Tanga Pharmaceutical & Plastics Limited kuwa alama iliyowasilishwa na Dream Cosmetics inafanana na yao.

Katika uamuzi wake, Msajili alisema: “Alama ya Dream Cosmetics inafanana na ile ya Tanga Pharmaceutical. Alama ya biashara ya ‘BABYMED’ huenda ikachanganywa na alama ya Tanga Pharmaceutical ya biashara ya ‘BABY & ME’.”

Muombaji wa jina hilo, Dream Cosmetics, hakuridhishwa na uamuzi huo na kuamua kukata rufaa namba 3098 ya 2025 katika Mahakama Kuu, Dar es Salaam, akiwa amejenga hoja katika sababu kuu mbili kupinga uamuzi huo.

Aliwasilisha sababu mbili, moja, kwamba Naibu Msajili alikosea kisheria na kimantiki kwa kuamua kuwa alama za ‘BABYMED’ na ‘BABY & ME’ zinafanana na zina uwezekano wa kudanganya au kusababisha mkanganyiko kwa watumiaji.

Mbili, kampuni hiyo ilidai kuwa Naibu Msajili alikosea kisheria na kimantiki kwa kuamua kuwa alama ya ‘BABY & ME’ ni alama inayojulikana sana.

Katika rufaa hiyo, mrufani ambaye ni kampuni ya Dream Cosmetics aliwakilishwa na wakili Honest Shio, wakati mjibu rufaa ambaye ni kampuni ya Tanga Pharmaceutical & Plastics Limited aliwakilishwa na wakili Paschal Kamala.

Wakili Shio alishikilia msimamo kuwa Msajili alikosea kwa kusema alama za ‘BABYMED’ na ‘BABY & ME’ zinafanana, akisema hakukuwa na uhalali wowote wa kuondoa herufi “D” na ishara (symbol) “&” ili alama hizo zionekane kufanana.

Wakili huyo alisema, kwa uchunguzi wake, ingawa zote zina neno ‘BABY’, ambalo halina upekee mkubwa chini ya daraja la 3, vipengele bainishi—ambavyo ni ‘&ME’ kwa mjibu rufaa na ‘MED’ kwa muombaji—pamoja na nembo zao, rangi, fonti na uwasilishaji wa jumla, huleta tofauti kubwa.

Kwa mujibu wa wakili huyo, Msajili alipaswa “kuvaa viatu vya mtu wa kawaida kabisa” (common man) na kuona kama kuna mfanano katika alama hizo mbili ambao utamfanya achukue bidhaa ambayo hakuikusudia, na kinyume chake.

“Naibu Msajili alishindwa kuzingatia alama hizo kwa ujumla wake, akilenga mfanano mdogo huku akipuuza tofauti kubwa za kimuonekano, kifonetiki na kimaana, kinyume na kanuni za kisheria zinazoongoza alama za biashara duniani,” alidai.

Kwa upande wake, wakili Kamala aliyewawakilisha wajibu rufaa aliwasilisha kuwa alama za ‘BABYMED’ na ‘BABY & ME’ zinafanana kwa namna inayoweza kutatanisha, hivyo haziwezi kusajiliwa chini ya kifungu cha 19 na 20 cha usajili wa alama za biashara.

Alieleza kuwa mjibu rufaa, kampuni ya Tanga Pharmaceutical, anamiliki haki za kipekee za chapa ya biashara ya ‘BABY & ME’, ikijumuisha haki zinazolindwa kupitia sheria mbalimbali za usajili wa alama za biashara nchini Tanzania na kimataifa.

Aliongeza kuwa alama ya biashara ya ‘BABY & ME’ ilisajiliwa nchini Tanzania mwaka 2011 kama TZ/T/2011/354, Class 3, kwa uainishaji wa kimataifa wa bidhaa na huduma, ikihusisha mafuta ya kupaka, ya nywele, losheni, poda na bidhaa zote za daraja la 3, na kwamba usajili huo bado ni halali.

Katika hukumu aliyoitoa Aprili 14, 2026, na kuwekwa katika tovuti ya mahakama Aprili 20, 2026, Jaji Awamu Mbagwa alisema hoja iliyopo mbele yake ni kuamua kama alama hizo zinafanana kiasi cha kuleta mkanganyiko kwa umma.

“Uchambuzi juu ya suala hilo utaonesha kama Msajili alikuwa sahihi kwa kukataa kuandikishwa kwa alama ya warufani ‘BABYMED’ Au la,” alisema.

Akirejea sheria, kifungu cha 2 na kesi mbalimbali zilizowahi kuamuliwa, Jaji alisema ni wazi kwamba alama ya biashara kwa ajili ya usajili lazima iwe tofauti na iweze kutofautishwa na bidhaa au huduma za mmiliki na za mtu mwingine.

“Ikumbukwe kwamba wakati mlalamikaji alipoomba kusajili alama ya biashara ‘BABYMED’, alama ya biashara ya mjibu rufaa, ya ‘BABY & ME’, ilikuwa kwenye rejista kwa takriban miaka 10, kuanzia 2011,” alisema.

Jaji aliongeza kuwa ni msingi wa kisheria kwamba sheria inakataza kusajili alama ya huduma au biashara inayofanana au inayokaribia kufanana na nyingine kiasi cha kuweza kuwachanganya walaji au watumiaji.

“Ni msimamo uliowekwa kwamba katika kutathmini iwapo alama hiyo inaweza kuwachanganya wananchi, mahakama inatakiwa kuvaa viatu vya mtu wa kawaida, kuangalia alama na kuzingatia iwapo mtu wa kawaida ana uwezekano wa kuchukua bidhaa isiyokusudiwa,” alisema Jaji katika hukumu hiyo.

“Sasa, swali hapa ni iwapo alama hizo mbili, yaani ‘BABYMED’ na ‘BABY & ME’, zinaweza kuwachanganya wateja. Kuna kanuni mbalimbali katika kuamua kufanana kwa alama za biashara na huduma,” aliongeza.

“Mojawapo ni ‘the anti-dissection rule’, ambapo alama zinazobishaniwa hutazamwa katika muonekano wake wa jumla bila kugawanya maneno.”

“Kwa kutumia kanuni hiyo, nimetathmini alama mbili—‘BABYMED’ na ‘BABY & ME’—kwa mtazamo wa mtumiaji wa kawaida. Pia nimezingatia kuwa alama zote mbili zinahusiana na bidhaa za daraja moja, yaani Daraja la 3.”

“Kama alivyosema Msajili, nina maoni thabiti kwamba alama hizi zinafanana kwa kiwango kinachoweza kuwachanganya watumiaji, na hivyo kuharibu madhumuni ya chapa ya biashara kama inavyopendekezwa chini ya kifungu cha 2 cha sheria.”

“Kwa kweli, mtumiaji wa kawaida anaweza kushindwa kutofautisha ‘BABYMED’ na ‘BABY & ME’. Kwa msingi huo, Msajili alikuwa sahihi kukataa kusajili chapa ya biashara ya ‘BABYMED’ wakati tayari kuna chapa yenye maneno ‘BABY & ME’,” alisisitiza.

Jaji alihitimisha kuwa, kwa uchambuzi huo, uamuzi wa Msajili ulikuwa sahihi na unaungwa mkono na sheria chini ya kifungu cha 20(1), na hivyo mahakama inabariki uamuzi huo na kutupilia mbali rufaa hiyo.