Dar es Salaam. Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi ameliomba Bunge kuidhinishia Sh2.52 trilioni katika mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele vitano vya wizara hiyo.
Vipaumbele hivyo ni kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme; kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia, kuendeleza sekta ya mafuta na gesi asilia pamoja na kuimarisha usalama wa nishati nchini.
Kati ya fedha hizo alizoomba, Sh2.462 trilioni sawa na asilimia 97.5 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo na Sh63.04 bilioni sawa na asilimia 2.5 za matumizi ya kawaida.
Bajeti hiyo ni ongezeko la asilimia 29, ukilinganisha na bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 unaoishia Juni 30, mwaka huu, ambayo ilikuwa ni Sh1.96 trilioni.
Ndejembi ameeleza hayo bungeni jijini Dodoma leo, Jumatano Aprili 22, 2026 alipowasilisha bajeti ya mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Amesema kipaumbele cha kwanza ni kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, ikiwamo kuunganisha mikoa ya Rukwa, Kagera, Lindi na Mtwara katika Gridi ya Taifa.
“Pia, tutaendelea kutekeleza mradi wa kuimarisha gridi ya Taifa (Gridi Imara), kufanya matengenezo ya miundombinu ya umeme na kuendelea na usambazaji wa umeme katika vitongoji,” amesema.
Amesema kipaumbele kingine ni kuongeza kasi ya kuunganisha umeme kwa wananchi ili kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii, ikiwamo migodi, kilimo, viwanda, shule, pampu za maji na vituo vya afya.
Katika eneo la miradi ya maendeleo, amesema fedha hizo pia zitagharamia utekelezaji wa miradi ya uzalishaji wa umeme ya Malagarasi, Julius Nyerere, Kakono na Kinyerezi I Extension, mradi wa umeme jua Shinyanga na mingine ya kimkakati.
Amesema Serikali pia imeweka kipaumbele katika kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024/34 na Mpango Mahususi wa Taifa wa Nishati wa mwaka 2025/30.
“Bajeti hii inalenga kuimarisha uzalishaji wa gesi asilia, kutekeleza miradi ya utafutaji na uendelezaji wa rasilimali hiyo, mradi wa LNG, mradi wa Ntorya na ya utafutaji katika vitalu vya Eyasi-Wembere, Lindi-Mtwara na Mnazi Bay,” amesema.
Amesema upatikanaji wa gesi asilia kwa matumizi ya viwandani, majumbani na vyombo vya moto kupitia CNG pia ni sehemu ya vipaumbele vinavyolengwa na fedha hizo.
Katika sekta ya mafuta, Ndejembi amesema bajeti hiyo itawezesha pia jitihada za kuimarisha miundombinu ya uhifadhi na usafirishaji wa mafuta ya petroli na kufuatilia hali ya upatikanaji wa nishati hiyo duniani.
Amesema sehemu ya fedha hizo itaelekezwa pia kuimarisha ushiriki wa wazawa katika shughuli za mafuta na gesi, kuboresha utendaji wa taasisi zilizo chini ya wizara na kuongeza tija na ufanisi katika utoaji wa huduma.
Ndejembi, amesema kati ya fedha za maendeleo zilizoombwa, Sh1.602 trilioni ni za ndani na Sh859.92 bilioni ni fedha za nje.