Sh39 bilioni kukamilisha mradi wa maji Njombe

Njombe. Zaidi ya Sh39 bilioni zinatarajiwa kukamilisha mradi wa maji wa miji 28 katika Halmashauri ya Mji wa Njombe, wenye lengo la kumaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa maeneo mbalimbali ya mji huo mkoani Njombe.

Kwa mujibu wa taarifa za utekelezaji, mradi huo ambao umefikia asilimia 60, unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni mwaka huu, ambapo wananchi wataanza kunufaika na huduma ya maji katika maeneo yao.

Hayo yamesemwa leo Jumatano, Aprili 22, 2026 na Msimamizi wa Mradi wa Maji wa Miji 28 kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Njombe (Njuwasa), Mhandisi Douglas Nkwama, wakati wa ziara ya ukaguzi iliyofanywa na mratibu wa Mbunge wa Njombe Mjini ili kujionea maendeleo ya mradi huo.

Msimamizi wa Mradi wa Maji Miji ishirini na nane Njombe, Douglas Nkwama akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Aprili 22, 2026 akiwa eneo la mradi huko Lunyanwi halmashauri ya mji wa Njombe

Mhandisi Nkwama amesema mkataba wa utekelezaji wa mradi huo ulisainiwa Juni 6, 2022, lakini ulichelewa kuanza kutokana na majadiliano ya chanzo cha maji kilichopaswa kutumika.

Amesema awali ilipangwa kutumia chanzo cha maji cha Mto Mgiwe, lakini baadaye uamuzi ulibadilishwa na kuruhusu matumizi ya chanzo cha Mto Hagafilo, hali iliyosababisha mradi kuanza rasmi Aprili 2024.

“Changamoto kubwa ilikuwa kuchelewa kuanza kwa mradi kutokana na mabadiliko ya chanzo cha maji, kutoka Mto Mgiwe kwenda Mto Hagafilo baada ya maamuzi ya kitaalamu,” amesema Nkwama.

Mradi wa Maji Miji ishirini na nane uliopo Lunyanwi Halmashauri ya mji wa Njombe.

Ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa mradi huo, maeneo yatakayohudumiwa ni pamoja na Mtaa wa Lunyanwi ambako pia kuna ofisi za serikali, Mji Mwema, Msete, Wende pamoja na Stendi Mpya ya Mabasi ya Njombe.

Kwa mujibu wake, hatua zote muhimu za ujenzi tayari zimekamilika, na kilichobaki ni kukamilisha kazi chache za mwisho licha ya changamoto ndogo ndogo za mvua zinazoendelea kunyesha.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mbunge wa Njombe Mjini, Crispin Kalinga amesema kukamilika kwa mradi huo kutaleta nafuu kubwa kwa wananchi wa kata mbalimbali za Njombe Mjini na maeneo jirani.

Amesema ziara hiyo ililenga kujiridhisha na taarifa zilizotolewa na wananchi wa Mtaa wa Mji Mwema kuhusu changamoto ya maji katika Stendi Kuu ya Mabasi ya Njombe.

“Kimsingi wananchi walikuwa na hofu kuwa maji ya stendi yanahudumiwa na NJUWASA, kumbe ni visima vya ndani ya stendi vinavyosimamiwa na uongozi wake,” amesema Kalinga.

Ameipongeza Njuwas kwa utekelezaji wa mradi huo mkubwa, akisema licha ya mvua zinazoendelea kunyesha, maendeleo ya mradi yanaridhisha na yanaonyesha uwezekano wa kukamilika kwa wakati.

Naye Ofisa Habari wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Ichikael Malisa amewatoa hofu wananchi kuhusu changamoto ya maji katika stendi hiyo, akieleza kuwa ilitokana na hitilafu za muda katika visima vilivyopo.

Mradi wa Maji Miji ishirini na nane uliopo Lunyanwi Halmashauri ya mji wa Njombe.

Amesema hatua za haraka zilichukuliwa baada ya taarifa kufikishwa kwa uongozi wa halmashauri, ambapo maji ya dharura yalipatikana ili kuhakikisha huduma haikatizwi kwa watumiaji wa stendi.

“Niombe wananchi wapuuze taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba watu wanatumia maji ya madimbwi, hazina ukweli wowote,” amesema Malisa.

Mkazi wa Njombe Mjini, Toinyo Kyando, amesema changamoto ya maji ilikuwepo awali lakini hatua zilizochukuliwa na viongozi ziliiwezesha kurejea kwa huduma hiyo muhimu.

Amesema kwa sasa huduma ya maji katika stendi hiyo imeimarika na wananchi wamepata nafuu baada ya tatizo hilo kushughulikiwa kwa haraka.