Sakata la Sowah Simba lawaibua vigogo wawili

BADO hakuna mwanga mzuri kwenye sakata la mshambuliaji Jonathan Sowah ambaye inaelezwa ameandika barua ya kutaka kuachana na Simba baada ya kusimamishwa na mabosi wa klabu hiyo, lakini sakata hilo limewaibua watu wawili wakiwa shauri Wekundu hao wa Msimbazi.

Tuanze na Evance Adotey ambaye ni kocha wa mwisho kuja na Sowah hapa nchini wakiwa wanafanya kazi pamoja pale Medeama ya Ghana, ameliambia Mwanaspoti viongozi wa Simba wanatakiwa kukaa chini na mshambuliaji huyo kujua changamoto zake ili awafanyie kazi vizuri.

Adotey amesema wakati akiwa na Sowah alikuwa kila akiona hafanyi vizuri anakaa chini na kutafuta changamoto zake na kuzipeleka kwa uongozi, kisha kutatuliwa na baada ya hatua hiyo mshambuliaji huyo alikuwa akionyesha uwezo mkubwa.

“Nimesikia Sowah ana shida na uongozi wake, sijaongea naye muda mrefu, ukiona Sowah hafanyi vizuri uwanjani ujue ana changamoto, hilo limetokea sana hapa tulipokuwa Medeama, nilikuwa nikimwona hayuko kwenye utulivu, nilikuwa namuita na kuongea naye,” amesema Adotey.

“Nikijua changamoto zake, nawaita viongozi wanazifanyia kazi, kama ni mambo ya ufundi nasimama mwenyewe kumrekebisha au kumfafanulia, ukweli ni Sowah ana kipaji kikubwa sana cha kufunga na wakati wote anapenda kuwa uwanjani.”

Wakati Adoyey akiyasema hayo, bosi wa zamani wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ amesema Sowah kipaji chake bado kilikuwa kinahitajika ndani ya kikosi chao na changamoto zake zilikuwa zinahitajika kujulikana mapema kisha kutafutiwa njia ya kumtuliza ili afanye kazi.

“Huko nyuma tulikuwa na wachezaji watukutu sana, lakini unahitaji utulivu kujua ni namna gani ya kuwafanya wafanye kazi vizuri,” amesema Kaburu.

“Sowah ilikuwa inajulikana kwamba ni mchezaji wa namna gani, wakati tunamsajili tulitakiwa kujua changamoto zake na hii ni kwa mchezaji yeyote, baada ya kujua hizo changamoto viongozi wangu walitakiwa kujua ni namna gani watamfanya ili timu ipate huduma ya kipaji chake kama ambavyo huko nyuma tulikuwa tunafanya kwa wachezaji wengine ambao walikuwa na shida kama hizi hasa wakati huu ambao tulikuwa tunataka mchezaji mwenye ubora mkubwa kule mbele.”

Sowah alisimamishwa na Simba kwa madai mbalimbali ya utovu wa nidhamu ambayo hata hivyo mshambuliaji huyo Mwanaspoti inafahamu kwamba aliyakanusha kwa maandishi ambapo bado uongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi haujamrudisha kundini.

Sowah ambaye mpaka anasimamishwa alifanikiwa kufunga mabao matatu Ligi Kuu Bara, Simba imekuwa inategemea nguvu ya mshambuliaji mmoja pekee Seleman Mwalimu aliyefunga mabao sita hadi sasa katika ligi hiyo.

Kabla ya Sowah kusimamishwa na Simba Februari mwaka huu, mshambuliaji huyo aliitumikia adhabu ya kukosa mechi tano kutokana na utovu wa nidhamu aliyopewa Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) baada ya kikao chake cha Desemba 15, 2025. Adhabu hiyo ilimalizika Februari 25, 2026.