Mgogoro kati ya Israel kwa kushirikiana na Marekani dhidi ya Iran umefikia hatua tata sana hadi sasa, licha ya mazungumzo ya kusitisha mapigano, vita bado haijamalizika wala kupata suluhisho la kudumu.
Hali ya sasa inaonesha mchanganyiko wa vita vya kijeshi, mashinikizo ya kisiasa, na kushindikana kwa diplomasia.
Hadi sasa, moja ya mambo makubwa yaliyofanya vita ishindikane kumalizika ni tofauti kubwa za kimkakati kati ya pande husika.
Israel imechukua msimamo mkali wa kuendelea na operesheni za kijeshi wakati Marekani inaonesha dalili za kutaka kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano. Israel inaonekana kuandaa kitu kama “vita ya muda mrefu” kwa kulianzisha kwenye maeneo kama Lebanon ili kuzuia uungwaji mkono kwa Iran.
Sababu nyingine kubwa ya kushindikana kumaliza vita ni kutokuelewana kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano. Kumekuwa na madai ya kila upande kukiuka makubaliano hayo. Kwa mfano, Iran imelaumu Israel kwa kuendelea kushambulia maeneo ya Lebanon, wakati Israel na Marekani wanadai kuwa Lebanon haikujumuishwa kwenye makubaliano ya kusitisha mapigano.
Tofauti hizi zimefanya makubaliano kuwa dhaifu na kutoafikiwa kwa wepesi. Hii inaonesha uwezekano wa vita kuendelea kwa muda mrefu tofauti na tulivyofikiri. Mpaka sasa hakuna upande uliopata ushindi kamili, lakini pia hakuna ulio tayari kushindwa au kukubali masharti ya mwingine.
Iran bado ina uwezo wa kujibu mashambulizi, Israel inaendelea na operesheni zake za kijeshi, na Marekani iko katikati. Kigagaziko hiki kinamaanisha uhaba na hatimaye ukosefu wa mafuta.
Uhaba wa mafuta ni tatizo linaloathiri dunia nzima. Athari zake ni nyingi zikiwamo kupanda kwa gharama za maisha, kupungua kwa uzalishaji na kuongezeka kwa mahitaji ya nishati. Aidha, utegemezi mkubwa wa mafuta kama chanzo kikuu cha nishati unachangia hali hii kuwa mbaya zaidi. Kwa hiyo vita dhidi ya Iran inachoreka kama mtu anayebomoa kisima pekee kinachompatia maji.
Tanzania kama nchi nyingine zinazoendelea, inategemea uagizaji wa mafuta kutoka nje. Jambo hili linaufanya uchumi wake kuwa katika hatari kutokana na mabadiliko ya bei katika soko la kimataifa.
Hayo yamepelekea viongozi wengi wa Afrika kubuni njia za kupunguza tatizo. Kwa upande wako, Mheshimiwa Rais ametangaza kupunguza ukubwa wa misafara yako ili kubana matumizi ya mafuta.
Niseme ukweli, umetugusa wengi sana kwa uamuzi huo. Waswahili wanasema “shombo mkinuka wote si shombo,” yaani msiba wa wote hauna maumivu makali kama ulivyo msiba wa peke yako.
Lakini pia umeibua mjadala mpana huku uswahilini, kuhusu namna bora ya kukabiliana na uhaba wa nishati nchini. Kila mmoja amehamasishwa na mwanzo wako, na sasa kuna haja ya kuchungulia haya machache.
Kwa kawaida ombi la mkuu ni amri kwa wadogo.
Uamuzi wako unaonekana kuwa wa mfano unaolenga kuhamasisha uwajibikaji si tu kwa viongozi wa juu tu, bali pia kwa taasisi za serikali na wananchi kwa ujumla. Katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa mafuta, bei kupanda, na mabadiliko ya tabianchi, hatua kama hizi zina umuhimu mkubwa sana.
Kupanda kwa bei ya mafuta kunaathiri moja kwa moja maisha ya wananchi. Gharama za usafiri huongezeka, bei za bidhaa hupanda kutokana na gharama za uzalishaji na usafirishaji, na hatimaye mfumuko wa bei huongezeka.
Hali hii huathiri zaidi wananchi wa kipato cha chini, ambao hutumia sehemu kubwa ya kipato chao katika mahitaji ya msingi. Hivyo basi, juhudi za kubana matumizi ya mafuta si suala la kifahari bali ni hitaji la lazima kwa ustawi wa jamii.
Hatua ya rais kupunguza msafara wake ni ishara ya uongozi wa mfano. Kwa muda mrefu, kumekuwa na malalamiko kuhusu matumizi makubwa ya rasilimali katika shughuli za serikali, hasa katika misafara ya viongozi.
Kupunguza idadi ya magari katika misafara si tu kunapunguza matumizi ya mafuta, bali pia kunapunguza gharama za matengenezo na uendeshaji wa magari hayo. Hatua hii inaonesha dhamira ya dhati ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima serikalini.
Ni muhimu kwa serikali nzima kuiga mfano huu. Wizara, taasisi na mashirika ya umma yanapaswa kupitia upya matumizi yao ya mafuta na kuweka mikakati ya kuyapunguza.
Hii inaweza kujumuisha kupunguza safari zisizo za lazima, kuhamasisha matumizi ya mikutano ya mtandao na kuimarisha usimamizi wa magari ya serikali.
Aidha, matumizi ya magari yanayookoa mafuta au yanayotumia nishati mbadala kama umeme yanapaswa kupewa kipaumbele.
Mbali na serikali, sekta binafsi na wananchi pia wana wajibu wa kushiriki katika juhudi hizi.
Kampuni zinaweza kuanzisha sera za kupunguza matumizi ya mafuta, kama vile kuratibu usafiri wa wafanyakazi au kuhimiza kazi za mbali.
Wananchi kwa upande wao wanaweza kutumia usafiri wa umma, kushirikiana magari au kutumia njia mbadala kama baiskeli kwa umbali mfupi.
Tanzania ina fursa kubwa katika nishati ya jua, upepo, na maji.
Uwekezaji katika sekta hizi unaweza kusaidia kupunguza gharama za nishati kwa muda mrefu na kuongeza uhakika wa upatikanaji wake.
