Iringa. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Iringa kimeanza ukurasa mpya wa uhai wa kisiasa kwa kufungua ofisi zake huku kikilenga kuimarisha uhusiano na wananchi na kuboresha utendaji wa ndani ya chama baada ya kuwa kifungoni.
Aprili 15, 2026, Mahakama ya Rufani ilibatilisha zuio la kutokufanya shughuli za kisiasa lililotolewa na Mahakama Kuu, Juni 10, 2025 kufuatia kesi ya madai ya mgawanyo wa rasilimali za chama baina ya Bara na Zanzibar.
Pia, Mahakama ya Rufani ilielekeza kesi hiyo iendelee kusikilizwa na jaji mwingine ambaye atatakiwa kuchunguza na kujiridhisha iwapo ilifunguliwa ndani ya muda au la kabla ya kuendelea na hatua nyingine. Kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa Jaji Hamidu Mwanga.
Hukumu ya Mahakama ya Rufani ilitolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani: Augustine Mwarija, Issa Maige na Abraham Mwampashi.
Kutokana na uamuzi huo, Chadema ambacho kilikuwa kifungoni kwa siku 309, tayari kimetangaza kuitisha kamati kuu Aprili 28 na 29 itakayofanyika makao makuu ya chama hicho, Mikocheni jijini Dar es Salaam, huku kikisisitiza kitaendelea kuwapigania wananchi.
Aidha, kiliagiza ofisi zote mikoani kufunguliwa na kuanza kazi.
Wanachama na wafuasi wa Chama mcha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa wakiwa ofisi ya Chadema Veta Manispaa na mkoani Iringa katika zoezi la kufungua ofisi ili kuendelea na majukumu kufuatia kufunguliwa kwa chama hicho Aprili 15, 2026. Picha na Christina Thobias
Jana Jumatatu, Aprili 20, 2026 katika eneo la VETA Manispaa ya Iringa, wanachama na viongozi walifungua ofisi na kufanya usafi pamoja na ukarabati.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Iringa, Leonard Kurujila amesema chama kimejipanga kuweka mikakati madhubuti ya kuwafikia wananchi moja kwa moja ili kusikiliza na kushughulikia changamoto zao.
Kurujila amesema kufunguliwa kwa ofisi hiyo ni mwanzo mpya kwa chama baada ya kipindi cha vikwazo cha siku 310, akisisitiza kuwa sasa wataongeza kasi ya shughuli za kisiasa na kijamii.
“Ofisi hii inaendelea kufanyiwa ukarabati unaojumuisha marekebisho ya milango iliyoharibika pamoja na mengineyo na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika ndani ya siku mbili hadi tatu,” amesema Kurujila.
Kurujila amesema miongoni mwa mikakati hiyo ni kuimarisha mawasiliano kati ya viongozi na wanachama, kuongeza ushiriki wa wanachama katika shughuli za chama pamoja na kujenga upya miundombinu ya chama.
“Na juhudi hizi zinalenga kuhakikisha chama kinakuwa karibu zaidi na wananchi huku tukijiweka katika nafasi nzuri ya kushiriki kikamilifu katika masuala ya kisiasa na maendeleo ya jamii mkoani Iringa,” amesema Kurujila.
Naye Katibu wa Chadema Wilayani Kilolo Iringa, David Mfugwa amesema kwa kipindi chote walizokuwa hawaruhusiwi kufanya kazi za kiutendaji zimeathiri chama hicho kwa kushindwa kukutana na kujadiliana.
Hata hivyo, amesema hali hiyo haijawaathiri kuwarudisha nyuma katika upambanaji wa chama chao.
“Sisi hatujarudi nyuma hata kidogo, kweli tumeathirika katika utendaji kazi wetu kwasababu tulikuwa haturuhusiwi kutumia rasilimali zetu za chama,” amesema Mfugwa na kuongeza:
“Juu ya hili imani ya taasisi hii inazidi kuhimarika zaidi kwasababu tunapopitia hekaheka hizi sisi ndio tunahimarika.”
Baadhi ya wanachama hao wa Chadema mkoani Iringa wamepongeza hatua hiyo wakisema ni mwanzo mzuri wa kurejesha nguvu ya chama na kuongeza mshikamano ndani ya chama na kukijenga zaidi.
Wanachama na wafuasi wa Chama mcha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa wakiwa ofisi ya Chadema Veta Manispaa na mkoani Iringa katika zoezi la kufungua ofisi ili kuendelea na majukumu kufuatia kufunguliwa kwa chama hicho Aprili 15, 2026. Picha na Christina Thobias
Wamesema uwepo wa ofisi utarahisisha uratibu wa shughuli na kuwapa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya chama.
“Tumerudi upya na tunataka kukijenga chama kiwe kipya zaidi na kuhakikisha tunapambana,” amesema Mzee Thadei, mmoja wa Wanachama Chadema mkoani Iringa