Afrika, dunia ijifunze kutokana na Rwanda

Miaka 32 imepita tangu mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi yaliyotokea Aprili 7, 1994 nchini Rwanda, lakini uzito wa tukio hilo bado unaendelea kuitikisa dhamiri ya dunia.

Leo hii, swali haliko tena katika kuelezea yaliyotokea, bali katika kutathmini kama dunia imejifunza vya kutosha kuzuia janga kama hilo lisijirudie.

Maadhimisho ya kumbukizi ya mauaji hayo yaliyopewa jina la Kwibuka 32, yanatoa nafasi ya kutafakari kwa kina, si tu kwa Rwanda, bali kwa nchi zote za Afrika na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla.

Katika maadhimisho yanayoendelea kufanyika nchini humo kwa siku 100 yaliyoanza Aprili 7, 2026 huku bendera zote nchini humo zikipepea nusu mlingoti, viongozi wa taifa hilo wanatoa ujumbe unaobeba funzo la kihistoria na onyo kwa dunia.

Aprili 7, 2026, Rais wa nchi hiyo, Paul Kagame akilihutubia Taifa sambamba na viongozi wengine wa kitaifa, walisisitiza kuwa kumbukumbu hiyo si ya kuomboleza pekee, bali ni jukwaa la kuhamasisha hatua madhubuti dhidi ya chuki, ubaguzi na upotoshaji wa ukweli. Kwao Wanyarwanda, historia ya mwaka 1994 ni ushahidi kwamba maafa makubwa ya kibinadamu huanza kwa hatua ndogo zinazopuuzwa. Wanasema chuki ndani ya Taifa haiji ghafla, bali hujengwa polepole

Hivyo, moja ya funzo muhimu kutoka Rwanda ni kwamba mauaji ya kimbari hayaanzi kwa mlipuko wa ghafla. Huanzia kwenye maneno, lugha ya chuki inayolenga kundi fulani, propaganda zinazopotosha ukweli na siasa zinazochochea mgawanyiko.

Hali hizi zikiachwa ziendelee bila kudhibitiwa, hujenga mazingira ya hatari yanayoweza kusababisha maafa makubwa.

Katika ulimwengu wa sasa, ambako mitandao ya kijamii imepanua wigo wa mawasiliano, hatari hii imeongezeka maradufu. Taarifa zisizo sahihi zinaweza kusambaa kwa kasi na chuki inaweza kupandikizwa kwa urahisi zaidi kuliko awali. Ndiyo maana viongozi wa Rwanda wameendelea kusisitiza kuwa mapambano dhidi ya itikadi ya chuki yanapaswa kuanza mapema, kabla hayajakomaa na kuwa tishio.

Kwa Afrika, ambako baadhi ya jamii bado zinaathiriwa na tofauti za kikabila, kidini au kisiasa, onyo hili lina umuhimu wa pekee. Historia inaonyesha kuwa tofauti hizi zinapotumiwa vibaya, huweza kugeuka kuwa chanzo cha migogoro mikubwa.

Kwa Rwanda, licha ya kupita kwa zaidi ya miongo mitatu tangu mauaji hayo yatokee, bado kuna changamoto katika kuhakikisha haki inatendeka kikamilifu.

Baadhi ya washukiwa wa mauaji ya kimbari bado wanaishi katika nchi mbalimbali duniani, hali inayozua maswali kuhusu uwajibikaji wa kimataifa.

Rwanda imeendelea kutoa wito kwa nchi mbalimbali kushirikiana katika kuwakamata wahalifu hao, kuharakisha kesi zinazohusiana na mauaji ya kimbari na kupambana na vitendo vya kukanusha au kupotosha historia. Wito huu hauhusu Rwanda pekee, bali unalenga kulinda misingi ya haki duniani.

Kwa sababu haki ni msingi muhimu wa amani. Bila uwajibikaji, majeraha ya kihistoria hubaki wazi na uwezekano wa kurudia makosa ya zamani huongezeka.

Kwa mantiki hiyo, haki haipaswi kuonekana kama suala la kitaifa pekee, bali kama wajibu wa pamoja wa jumuiya ya kimataifa.

Kwa nchi za Afrika Mashariki, zikiwamo Tanzania na Kenya, maadhimisho ya Kwibuka yana umuhimu wa karibu zaidi.

Haya si matukio ya mbali yanayohusu historia ya taifa jingine pekee, bali ni kioo kinachoonyesha hatari zinazoweza kujitokeza popote pale ambapo chuki na mgawanyiko vinapopewa nafasi.

Katika muktadha huu, maswali muhimu yanapaswa kuulizwa; Je, mifumo ya kisiasa inalinda umoja wa kitaifa au inachochea mgawanyiko? Je, kuna mifumo madhubuti ya kudhibiti hotuba za chuki, hasa katika zama za teknolojia ya kidijitali? Na je, historia inafundishwa kwa uaminifu ili vizazi vijavyo vijifunze kutokana na makosa ya zamani?

Majibu ya maswali haya yanaweza kuamua mustakabali wa amani katika kanda hii. Kupuuza dalili ndogo za chuki kunaweza kuwa mwanzo wa matatizo makubwa.

Pamoja na historia yake ya maumivu makubwa, Rwanda imeonyesha uwezo wa kujijenga upya na kuwa mfano wa mafanikio barani Afrika. Kupitia sera za maridhiano, umoja wa kitaifa na maendeleo ya kiuchumi, taifa hilo limeweza kurejesha mshikamano wa kijamii na kujenga taasisi imara.

Hatua hizi zimeifanya kuwa mfano wa jinsi taifa linaweza kuinuka kutoka kwenye maangamizi na kujenga mustakabali mpya. Hata hivyo, viongozi wa nchi hiyo wanaendelea kusisitiza kuwa mafanikio haya hayaondoi umuhimu wa kuendelea kukumbuka historia.

Kumbukumbu ni sehemu muhimu ya uponyaji. Inasaidia jamii kuelewa yaliyopita, kujifunza kutokana nayo na kujenga mustakabali ulio bora zaidi.

Katika dunia ya sasa, changamoto ya upotoshaji wa taarifa imekuwa kubwa zaidi. Kuna juhudi za makusudi katika baadhi ya maeneo kupotosha au kukanusha ukweli wa matukio ya kihistoria, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kimbari ya Rwanda.

Hali hii ikiwa haitadhibitiwa inaweza kudhoofisha juhudi za maridhiano, kupotosha vizazi vijavyo na hata kufungua milango ya kurudia migogoro.

Akizungumza na Mwananchi, Felix Ndyekizibha mchambuzi wa masuala ya siasa nchini Rwanda anasema ndiyo maana jumuiya ya kimataifa, ikiwamo Umoja wa Mataifa, inaendelea kusisitiza umuhimu wa kulinda ukweli wa historia.

Ndyekizibha anasema hiyo itasaidia kupambana na upotoshaji wa historia jukumu ambalo ni la pamoja linalohitaji ushirikiano wa serikali, taasisi za elimu, vyombo vya habari na wananchi kwa ujumla.

‘Kamwe Tena’ iwe vitendo, si maneno, Ndyekizibha anasema kauli ya ‘Kamwe Tena’ imekuwa ikirudiwa kila mwaka katika maadhimisho ya Kwibuka.

Hata hivyo, anasema kauli hiyo haitakuwa na maana kama haitatafsiriwa kwa vitendo.

“Ni lazima kupambana na hotuba za chuki, kuwawajibisha wanaosambaza propaganda hatari, kuimarisha elimu ya historia na kujenga taasisi imara za haki,” anasema.

Anasisitiza ipo haja ya kuendeleza juhudi za kukuza umoja wa kitaifa na mshikamano wa kijamii.

Anasema kwa kufanya hivyo, ndipo kauli ya ‘Kamwe Tena’ itakapopata maana halisi kama ahadi ya dhati ya kulinda maisha ya binadamu.

Kwibuka 32 inatukumbusha kuwa amani haiwezi kudumu bila haki, na umoja hauwezi kujengwa bila juhudi za makusudi kwa sababu inasisitiza kwamba historia isipoeleweka na kuchukuliwa hatua, inaweza kujirudia. Kwa Afrika na dunia kwa ujumla, maadhimisho hayo ni zaidi ya kumbukumbu, ni onyo linaloishi na inakumbusha kuwa chuki inaweza kujengwa polepole, ukimya unaweza kuwa hatari na haki isipotendeka, maafa yanaweza kujirudia.

Changamoto si kukumbuka tu yaliyopita, bali kuhakikisha mifumo ya kisiasa, kijamii na kisheria inalinda utu wa binadamu wakati wote. Kumbukumbu hizi zinapaswa kuwa chachu yalichukua hatua na haki iwe msingi wa amani na umoja uwe nguzo ya maendeleo endelevu.