WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA ATOA WITO KURIPOTI UNYANYASAJI, ATAJA ARDHI KUONGOZA MALALAMIKO

…………

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema kuwa changamoto kubwa zinazowasilishwa na wananchi kupitia kituo cha huduma kwa wateja ni migogoro ya ardhi, masuala ya mirathi pamoja na ndoa za utotoni, huku akibainisha kuwa migogoro ya ardhi ndiyo inayoongoza kwa wingi wa malalamiko.

Akizungumza leo Aprili 15, 2026 jijini Dodoma baada ya kupokea simu na jumbe kutoka kwa wananchi mbalimbali, Dkt. Homera amesema serikali kupitia wizara yake imeweka utaratibu wa kushirikiana na wizara nyingine husika ili kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Amesema kituo hicho kinatoa fursa kwa wananchi kuwasiliana moja kwa moja na wizara kupitia programu maalum ya “Ongea na Waziri” inayofanyika mara tatu kwa mwezi, ambapo wananchi huwasilisha kero zao kwa njia ya simu, WhatsApp, barua pepe na hata kwa maandishi.

“Baada ya kupokea changamoto hizi, tunazichakata kwa njia mbalimbali; baadhi tunazijibu papo hapo, nyingine tunazifuatilia kwa maandishi, na zipo zinazohitaji usuluhishi ambapo wahusika huitwa wizarani kwa majadiliano zaidi,” amesema Dkt. Homera.

Aidha, ameeleza kuwa licha ya juhudi hizo, bado kuna changamoto kubwa ya unyanyasaji wa kijinsia ndani ya familia ambapo waathirika, hususan wanawake, hushindwa kutoa taarifa kwa hofu ya kuvunjika kwa ndoa zao.

“Watu wanapigwa na kunyanyaswa majumbani mwao lakini wanakaa kimya. Ni muhimu kutoa taarifa hata kwa siri kwa viongozi wa serikali za mitaa au madiwani ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa,” alisisitiza.

Alionya kuwa ukimya huo unaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kupoteza maisha, na kusisitiza umuhimu wa wananchi kuwa wazi pale wanapokumbana na changamoto hizo.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, zaidi ya simu 20 zimepokelewa katika siku hiyo, ambapo asilimia kubwa zilihusu migogoro ya ardhi, huku zilizobaki zikihusu mirathi, ndoa na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.

Aliongeza kuwa hali hiyo inaonesha bado kuna haja kubwa ya kuendelea kutoa elimu kwa umma ili kuwahamasisha wananchi kutorundika matatizo moyoni, bali wayawasilishe mapema ili yapatiwe ufumbuzi.

Dkt. Homera aliahidi kuwa wizara yake itaendelea kushirikiana na wadau wote wa sekta ya sheria, wakiwemo wanasheria, mawakili na mihimili ya mahakama, kuhakikisha haki inapatikana kwa wote na kero za wananchi zinapatiwa majibu kwa wakati.