Wanne mbaroni kwa tuhuma za kuchoma moto nyumba ya mzee wa miaka 70

Njombe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linawashikilia watu wanne, wakazi wa Kijiji cha Nduramo, wilayani Makete, kwa tuhuma za kuchoma moto nyumba ya Melania Swallo (70), kwa madai ya kuhusishwa na imani za kishirikina.

Aidha, jeshi hilo linawashikilia jumla ya watuhumiwa 36 kwa makosa mbalimbali, yakiwemo mauaji, wizi, uvunjaji na ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Aprili 15, 2026, katika makao makuu ya Polisi Mkoa wa Njombe, Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Mahamoud Banga amesema tukio hilo linadaiwa kusababishwa na imani za kishirikina, ambapo watuhumiwa wanamtuhumu Melania kuwa mchawi na kumhusisha na kupotea kwa ndugu yao katika mazingira ya kutatanisha.

Kamanda Banga amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Festo Jason Mahenge (48), Mirika Yosia Mahenge (26), Yosia Kalaso Mahenge (60) na Epesi Elias Tweve (38), wote wakazi wa kijiji cha Nduramo, wilayani Makete, mkoani Njombe.

“Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara utakapokamilika, basi watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa hatua zingine za kisheria,” amesema Banga.

Aidha, Jeshi la Polisi linamshikilia Feni Kabenelo Ngao (33), mfanyabiashara na mkazi wa Malembuli, wilayani Makete, kwa tuhuma za mauaji yaliyotokea Januari 6, 2026, ambapo alikuwa ametoroka baada ya tukio hilo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi, katika tukio hilo watu wawili, Wema Mwakoko (26) na Laiko Chengula (30), waliuawa kwa tuhuma za wizi, baada ya mtuhumiwa huyo, kwa kushirikiana na wenzake, kujichukulia sheria mkononi.

Vilevile, jeshi hilo linawashikilia Ziada Mrisho (37) na Julius Kilawa (29), wakazi wa mtaa wa Kambarage, Halmashauri ya Mji wa Njombe, kwa kukutwa na fedha bandia za dola za Marekani 700.

Inadaiwa kuwa iwapo wangekamilisha mpango wao wa kuzibadilisha, wangeweza kujipatia takribani Sh1.8 milioni.

Kamanda huyo ameongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana na mamlaka za kifedha, ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania, katika uchunguzi wa tukio hilo, na kwamba mara utakapokamilika, watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani.

Amesema katika jitihada za utoaji elimu kwa umma, Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwafikia wananchi kupitia shule, nyumba za ibada na vyombo vya habari, kwa lengo la kuwapa uelewa kuhusu namna ya kutambua na kuzuia uhalifu katika maeneo yao.

Kwa upande wa usalama barabarani, amesema kikosi cha usalama barabarani kimefanikiwa kupunguza makosa yanayochangia ajali kwa kutoa elimu kwa madereva, wamiliki wa vyombo vya moto pamoja na wananchi kwa ujumla.

Ameeleza kuwa jumla ya madereva 6,053 walikamatwa kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani, ambapo madereva 6,051 waliandikiwa faini. (Idadi ya madereva waliofungiwa leseni haikujumuishwa).

Aidha, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi au kufanya uharibifu wa mali, likisisitiza kuwa halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayejihusisha na vitendo vya uhalifu.