KOCHA Mkuu wa Uhamiaji, Abdul Saleh, amekiri kusikitishwa na matokeo ya kufungwa 3-0 na Raskazone katika mechi ya Kombe la FA Kanda ya Unguja hatua ya 16 bora, huku lawama zote akiziacha kwa wachezaji wa kikosi hicho.
Uhamiaji inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar, imetupwa nje ya mashindano hayo na Raskazone iliyopo Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja baada ya kupokea kipigo hicho Aprili 13, 2026 kwenye Uwanja wa Mao B, Unguja.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar, Uhamiaji ipo nafasi ya nne ikivuna alama 39 kwa michezo 22, huku Raskazone ikishika nafasi ya pili na pointi 55 katika msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza Unguja.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa Uhamiaji, Abdul Saleh, alisema: “Wakati wachezaji wapo uwanjani walionekana hawapo sawa kisaikolojia hali ambayo ilinifanya nijaribu kuwarudisha mchezoni bila mafanikio.”
Wakati kocha huyo akisema wachezaji walionekana kutokuwa sawa kisaikolojia, chanzo kutoka ndani ya timu hiyo kimeliambia Mwanaspoti kwamba kuna madai ya mgomo baridi.
“Wapo watu ambao hawaitakii mazuri timu na kuna sintofahamu inayoendelea ikiwa na lengo la kuwatoa wachezaji mchezoni,” kimesema chanzo kutoka ndani ya timu hiyo.
Wakati huohuo, vita ya timu za Ligi Daraja la Kwanza Unguja zilipokutana kwenye Uwanja wa Mao A kuwania kufuzu robo fainali ya Kombe la FA, ilimalizika kwa Black Sailors kuitembezea dozi Kundemba ya mabao 2-0, yaliyofungwa na Msati Kassim ambaye pia alitoa asisti ya bao la pili kwa Mustafa Omar ‘Vardy’.
Ushindi huo wa Black Sailors haukuwa rahisi kwani kipindi cha kwanza matokeo yalikuwa 0-0, ndipo kipindi cha pili wachezaji wa kikosi hicho wakakaza msuli na kufuzu robo fainali.