MWANAMKE KIMARA KIZIMBANI KWA UTAPELI WA Sh. MILIONI 60

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv 

MWANAMKE  Monica Beda (36), mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kiasi cha shilingi milioni 60.

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo leo Aprili 20,1026 na Wakili wa Serikali Cathbert Mbiling’i  imeileza mahakama kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Novemba 8, 2025, katika Mtaa wa Samora, jijini Dar es Salaam.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Salome Mshasha, imedaiwa mshtakiwa alimlaghai Agrey Festo Mashanda kwa kujifanya angeweza kumuagizia gari aina ya Mitsubishi Fuso Fighter Damper lenye chassis namba  FK418F-550031, huku akijua kuwa si kweli.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka  upelelezi wa shauri hilo umekamilika na wameomba kupangiwa tarehe kwa ajili ya usikilizwaji wa awali (PH).

Hata hivyo mshtakiwa amekana kutenda kosa hilo na amerudishwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana 

Mahakama ilimpatia mshtakiwa dhamana kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, ambapo mmoja wao anatakiwa kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika au fedha taslimu yenye thamani ya nusu ya fedha anazodaiwa kuiba, sawa na shilingi milioni 30.

Kesi hiyo limeahirishwa hadi Mei 6, 2026 kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali.