BAADA ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Polisi katika Ligi Kuu Zanzibar, sasa KVZ imebadilisha upepo na nguvu zote kuhamishia kwenye Kombe la Muungano.
KVZ ni mongoni mwa timu nne zilizopata nafasi ya kuiwakilisha Zanzibar katika michuano hiyo sambamna na Mlandege, Mafunzo na Muembe Makumbi.
Kombe hilo linatarajiwa kuanza leo Jumanne saa 1:15 usiku kwa mchezo mmoja kati ya bingwa mtetezi, Yanga dhidi ya Muembe Makumbi ambapo mtanange huo utachezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Mara kwa mara viongozi wa timu hiyo wamesikika wakisema kuwa wanahitaji kubeba mataji matatu msimu huu ikiwemo Ligi Kuu ya Zanzibar, FA na Muungano.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa KVZ, Abduljalil Mohamed, amesema kutokana na ubora wa timu hiyo, mipango yao ni kuifunga Azam na kufuzu nusu fainali.
Amesema, timu imefanya uwekezaji wa kuleta mabadiliko ndani ya ligi na ushindani kwa wapinzani wake wote watakaokutana nao lakini kwasasa inaanza na Azam.
“Tumejipanga vizuri kuhakikisha tunawapa ushindani wa kutosha Azam FC na hiyo sio mechi kwao upande wao, badala yake ni fainali, hivyo ijipange kuwa KVZ itakayokutana nayo sio wanayoifikiria,” amesema.
Amesema, kawaida ya fainali ni mawili kushinda au kushindwa, hakuna sare, kwa maana hiyo watahakikisha kuwa wanacheza mpira wenye kiwango kizuri na kitakacholeta matokeo mazuri upande wao.
Mtanage huo kati ya KVZ na Azam utachezwa kesho Jumatano Aprili 22, saa 1:15 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.
Msimu uliopita KVZ iliishia hatua ya robo fainali ya mashindano hayo baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Yanga, mechi iliyochezwa Uwanja wa Gombani uliopo kisiwani Pemba.
