Dar es Salaam. Mfanyabiashara na mkazi wa Kimara, Monica Beda (36) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa shtaka moja la kujipatia Sh60 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Beda anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka kwa Agrey Mashanda, kwa madai kuwa atamuagizia gari aina ya Mitsubishi Fighter Fuso.
Mshtakiwa amefikishwa mahakamani hapo leo Jumatatu Aprili 20, 2026 na kusomewa kesi ya jinai namba 8385 ya mwaka 2026 na wakili wa Serikali, Cathbert Mbiling’i mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Salome Mshasha
Mbiling’i amedai mshtakiwa anadaiwa Novemba 8, 2025 Mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam, kwa njia ya udanganyifu Beda alijipatia fedha taslimu Sh60 milioni kutoka kwa Agrey Mashanda.
Alijipatia fedha hizo kutoka kwa Mashanda kwa maelezo kuwa utamuagizia gari aina ya Toyota Mitsubishi Fighter Fuso, wakati ukijua kuwa ni uongo.
Mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka hilo, alikana kutenda kosa hilo.
Upande wa Jamhuri umedai kuwa upelelezi wa kesi umekamilika na wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea maelezo ya awali (Ph).
Hakimu Mshasha amesema shtaka linamkabili mshtakiwa lina dhamana na kisha kutoa masharti ya dhamana.
Amesema mshtakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili na mmojawapo anatakiwa awasilishe nusu ya mali anayodaiwa kuiba ambayo ni Sh30 milioni au awasilishe mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Hakimu Mshasha amesema kama wadhamini wataweka hati ya kiwanja kama dhamana, hati hiyo inatakiwa iwe imefanyiwa tathimini na ripoti yake kuambatanishwa kwa pamoja.
Pia wadhamini hao wanatakiwa wawe na barua za utambulisho kutoka taasisi husika kama ni wafanyakazi na kama sio wafanyabiashara wawe na barua kutoka serikali za mitaa.
Mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana hivyo amepelekwa rumande.
Hakimu Mshasha ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 6, 2026 kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.
